Israel yashambulia bandari ya Hodeidah
6 Mei 2025Kulingana na taarifa ya jeshi la Israel iliyotolewa Jumanne, jeshi hilo limeshambulia kile ilichokiita kuyalenga maeneno ya magaidi wa Kihouthi katika mji wa Hodeidah na viunga vyake, likidai kuwa bandari hiyo ilikuwa inatumika kusafirisha silaha za Iran na zana nyingine za kijeshi.
Likivinukuu vyanzo vya habari vya wizara ya afya, shirika la habari la Saba linaloendeshwa na Houthi limeripoti kuwa mashambulizi hayo yaliyofanyika Jumatatu yamewaua watu watatu na kuwajeruhi wengine wapatao 39, katika mashambulizi sita kwenye bandari ya Hodeidah na shambulizi jingine katika wilaya ya Bajil. Aidha, waasi hao wamezilaumu Marekani na Israel kwa uchokozi.
Mashambulizi yamesababisha madhara makubwa
Vyanzo vinginne vitatu vya habari, vimeeleza kuwa waasi wa Kihouthi walilifunga eneo karibu na bandari na kiwanda cha saruji kutokana na mashambulizi hayo. Waasi hao wamesema kiwango cha uharibifu katika bandari bado hakijulikani, lakini ukubwa wa mashambulizi na moto ulisababisha madhara makubwa kwenye maeneo yanakohifadhiwa makontena.
Mfanyakazi mmoja katika kiwanda cha saruji, Osama Mohammed Mohammed al-Dhiabi amesema mashambulizi hayo yametokea wakati wa muda wa maombi ya jioni. ''Bado sijajua ni wangapi, lakini kuna wafanyakazi ndani ya kontena. Kuna majeruhi hospitalini, wengine mashahidi, wengine wana majeraha ya moto, na wote ni raia. Hiki ni kiwanda cha kiraia, hakina silaha. Kuna wafanyakazi wasio na hatia,'' alifafanua Osama.
Katika hatua nyingine, Iran imelaani vikali mshambulizi hayo ya anga ya Israel katika bandari ya Hodeidah. Akizungumza Jumanne, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amelaani shambulizi hilo akisema kuwa ni uhalifu wa wazi na ukiukaji mkubwa wa kanuni na sheria za kimataifa. Baqaei amezisihi mamlaka za kimataifa na nchi zenye nguvu kikanda kuchukua hatua dhidi ya kile alichokiita ''uharibifu'' unaondelea wa Marekani na Israel katika mataifa ya Kiislamu. Hata hivyo, afisa wa Marekani amekanusha nchi hiyo kuhusika katika mashambulizi hayo.
Soma zaidi: Israel na Wahouthi washambuliana kwa makombora
Wakati huo huo, afisa wa ngazi ya juu wa Hamas, Basem Naim amesema kundi hilo halina tena nia ya kufanya mazungumzo ya kusitisha mapigano na Israel na limeitaka jumuia ya kimataifa kuhakikisha vita vya Israel dhidi ya Gaza vinamalizika. Naim ameliambia Jumanne Shirika la Habari la Ufaransa, AFP kuwa hakuna maana yoyote ya kushiriki katika mazungumzo au kuzingatia mapendekezo mapya ya kusitisha mapigano, ikiwa vita vinaendelea katika Ukanda wa Gaza.
Soma zaidi: Israel yatanua kampeni ya kijeshi Gaza
Kulingana na afisa huyo mwandamizi wa Hamas, ulimwengu unapaswa kuishinikiza serikali ya Israel ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kumaliza uhalifu wa njaa, kiu, na mauaji katika Ukanda wa Gaza. Naim ameyatoa matamshi hayo siku moja baada ya jeshi la Israel kusema oparesheni iliyoongezwa huko Gaza, itajumuisha kuwaondoa wakaazi wake wengi.
(AFP, AP, Reuters)