Israel yasema Uhispania yaendesha chuki dhidi ya Wayahudi
8 Septemba 2025Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar ameilaumu Uhispania kwa kuendeleza kampeni ya chuki dhidi ya Wayahudi baada ya Waziri Mkuu Pedro Sanchez kutangaza hatua tisa zinazolenga kukomesha alichokisema "mauaji ya kimbari huko Gaza".
Uhispania imekanusha vikali shutuma za Israel na imeziita kuwa ni za uwongo kuhusu Uhispania kuwa na chuki dhidi ya taifa la Israel na Wayahudi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uhispania pia imelaani hatua ya Israel ya kuwapiga marufuku mawaziri wake wawili kuingia nchini Israel ikisema Uhispania haitatishwa katika juhudi zake za kutetea amani, sheria za kimataifa na haki za binadamu.
Kuhusu mashambulizi ya risasi yaliyofanyika katika mji wa Jerusalem Jumanne asubuhi idadi ya watu waliofariki imeongezeka na kufikia watu sita. Kulingana na wahudumu wa afya, wahasiriwa ni wanaume watano na mwanamke mmoja
Watu wanne walitangazwa kufariki katika eneo la tukio huko kaskazini mwa Jerusalem na baadae mwanamume mmoja na mwanamke walifariki hospitalini kutokana na majeraha waliyopata.
Watu wengine kumi na mbili waliojeruhiwa walipelekwa hospitalini, na saba kati yao wamepata majeraha makubwa na wako katika hali mahututi.
Polisi wamesema watu wawili walifika kwa gari kwenye eneo la makutano la Ramot katika jiji la Jerusalem na kufyatua risasi kuelekea kwenye kituo cha basi na mara moja afisa wa usalama na raiawaliokuwepo kwenye eneo la tukio walijibu kwa kuwafyatulia risasi kuwazuia washambuliaji kuendelea na kuwashambulia watu.
Wakati huo huo Israel kupitia waziri wake wa Mambo ya Nje Gideon Saar imesema imekubali pendekezo la Marekani la kusitisha vita huko Gaza. Saar amesema:
"Rais Trump alisema wazi Jumapili, kwamba Israel imelikubali pendekezo lake. Tuko tayari kuyapokea makubaliano kamili ambayo yatamaliza vita kwa kuzingatia uamuzi wa baraza letu la mawaziri. Lakini mambo mawili lazima yafanyike. La kwanza, kurejeshwa kwa mateka wetu. Na jambo la pili, ni kwamba Hamas lazima wakubali kuweka silaha zao chini."
Akijibu, afisa mkuu wa Hamas Basem Naim, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kundi lake halitaweka chini silaha zake bali litawaachilia mateka wote iwapo Israel itakubali kusitisha vita na kuviondoa vikosi vyake kutoka Gaza, na huo kwa muda mrefu ndio umekuwa msimamo wa kundi la wanamgambo wa Palestina la Hamas.
Vyanzo: AFP/DPA