Israel yasema imemuua msemaji wa kijeshi wa Hamas Abu Abeida
31 Agosti 2025Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amethibitisha Jumapili kwamba msemaji wa muda mrefu wa kijeshi wa Hamas, Abu Obeida, ameuliwa katika shambulizi la anga mjini Gaza. Kupitia ujumbe aliouandika kwenye X, Katz aliwapongeza wanajeshi wa Israel na idara ya usalama wa ndani, Shin Bet, kwa "utekelezaji bora bila kasoro.”
Abu Obeida, ambaye jina lake halisi ni Hudaifa al-Kahlut kwa mujibu wa jeshi la Israel, alikuwa sauti kuu ya kitengo cha kijeshi cha Hamas, Qassam Brigades. Alijulikana kwa kujifunika uso kwa kitambaa cha rangi nyekundu na kuzungumza kupitia video na sauti zilizotolewa na Hamas.
Hamas, kwa upande wake, haijatoa tamko rasmi kuthibitisha kifo chake. Baadhi ya viongozi wake wameyataja madai haya kuwa ni "vita vya kisaikolojia” vinavyolenga kudhoofisha ari ya wapiganaji na raia wanaoendelea kukabiliana na mashambulizi.
Hospitali za Gaza zimeripoti kwamba angalau watu 43 wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu Jumamosi, wengi wao wakiwa raia waliokimbilia maeneo yanayodhaniwa kuwa salama. Mashirika ya kibinadamu yanasema idadi hiyo huenda ikaongezeka kutokana na ugumu wa kufika maeneo yaliyoathirika.
Takwimu kutoka wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas zinaonyesha kwamba zaidi ya watu 63,000 wamefariki katika vita vya sasa, wengi wao wakiwa raia, takwimu ambazo Umoja wa Mataifa unaziona kuwa za kuaminika.
Operesheni za kijeshi na athari zake Gaza
Wakati akihutubia kikao cha baraza la mawaziri, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema shambulizi hilo lilikuwa sehemu ya operesheni maalum ya pamoja kati ya jeshi la ulinzi la Israel (IDF) na idara ya Shin Bet. Hata hivyo, alikiri kwamba bado hawajapata uhakika kamili kuhusu matokeo ya mwisho ya shambulizi hilo.
Mashambulizi ya anga yameendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya Gaza City, huku moshi mzito ukifunika anga ya jiji hilo. Wakazi waliokuwa wakihifadhiwa kwenye kambi za muda walieleza kuwa walishuhudia "hofu, moto na uharibifu mkubwa” katika mabanda yao baada ya mashambulizi ya usiku wa kuamkia Jumapili.
Katika mahojiano na AFP, Iman Rajab, mmoja wa walioko kwenye kambi karibu na Gaza City, alisema, "Tunaogopa usiku na kulala hemani. Tumechoka na hofu, njaa na kukimbia makazi yetu mara kwa mara.” Umoja wa Mataifa unasema karibu wakazi milioni moja bado wako katika jiji na vitongoji vyake, huku kukiwa na hali ya njaa iliyoelezwa kama "ya janga.”
Mashirika ya uokoaji yamesema mashambulizi ya anga na mashambulizi ya risasi katika maeneo mbalimbali Jumapili yalisababisha vifo vya angalau watu 24, wakiwemo 15 waliokuwa karibu na maeneo ya kugawia misaada. Jeshi la Israel limesema litahitaji uratibu zaidi ili kuthibitisha taarifa hizo.
Kwa sasa, upatikanaji wa habari huru kutoka Gaza umekuwa mgumu kutokana na vizuizi dhidi ya vyombo vya habari na hali tete za kiusalama, jambo linalofanya iwe vigumu kuthibitisha idadi kamili ya vifo na uharibifu unaoripotiwa.
Mapigo kwa uongozi wa Hamas
Kifo cha Abu Obeida ni mwendelezo wa operesheni za Israel zinazolenga viongozi waandamizi wa Hamas. Hapo awali, Israel iliwaua viongozi wengine wakuu akiwemo Yahya Sinwar, aliyekuwa akichukuliwa kama mpangaji mkuu wa mashambulizi ya Oktoba 7, 2023, na Ismail Haniyeh, kiongozi wa kisiasa wa Hamas, pamoja na kamanda wa kijeshi Mohammed Deif.
Vifo hivi vimetikisa muundo wa uongozi wa Hamas na kupelekea pengo kubwa katika safu za juu za kundi hilo, ingawa wachambuzi wanaonya kwamba bado kuna wanachama wa ngazi za chini na za kati wanaoendeleza operesheni.
Mashambulizi hayo yamefanywa sambamba na mashinikizo ya kimataifa yanayoitaka Israel kupunguza kasi ya mashambulizi kutokana na vifo vya raia na hali mbaya ya kibinadamu Gaza, ambapo Umoja wa Mataifa umeonya kuwa zaidi ya watu nusu milioni wanakabiliwa na hali ya "janga”
Wakati huo huo, takwimu zinaonyesha kuwa watu 1,219 waliuawa nchini Israel kufuatia mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, huku mateka 251 wakichukuliwa hadi Gaza. Idadi ya waliobaki hai inakadiriwa kuwa karibu watu 20, huku wengine wengi wakiwa bado hawajulikani walipo.
Israel imeendelea kusisitiza kuwa kampeni yake inalenga "kuiangamiza kabisa Hamas” na kuwarejesha mateka wake, ingawa mashirika ya haki za binadamu yamesema mashambulizi yamekuwa na athari kubwa kwa raia wasiokuwa na uhusiano na mapigano.
Mwelekeo wa baadaye na vitisho vipya
Mkuu wa Majeshi ya Israel, Luteni Jenerali Eyal Zamir, alisema Jumapili kuwa operesheni dhidi ya viongozi wa Hamas itaendelea hata nje ya Gaza. "Huu si mwisho. Viongozi wengi wa Hamas wako nje ya Gaza, na tutawafikia huko pia,” alisema, akithibitisha mpango wa kupanua operesheni za kijeshi kimataifa.
Taarifa hiyo imezua hofu mpya kwamba mashambulizi ya kulenga viongozi wa Hamas yanaweza kuongezeka katika mataifa ya Mashariki ya Kati na hata Ulaya, maeneo ambako baadhi ya viongozi wa kundi hilo wameripotiwa kuishi kwa muda mrefu.
Wakati hayo yakiendelea, mashirika ya kibinadamu yanaonya kuwa hali ya Gaza inazidi kuwa mbaya zaidi. Umoja wa Mataifa umetangaza rasmi hali ya njaa, na hospitali zimeripoti kuwa hazina vifaa vya kutosha kuokoa maisha ya maelfu ya watu walioko katika hali mbaya.
Kwa upande wa kisiasa, vifo vya viongozi wa Hamas vinachukuliwa na serikali ya Israel kama ushindi mkubwa, lakini wachambuzi wanasema vinaweza pia kuongeza ukinzani na kuchochea upinzani wa silaha, jambo linaloweza kuongeza muda wa vita na kuendelea kuathiri raia.
Katika mazingira haya magumu, wito wa jumuiya ya kimataifa wa kusitisha mapigano na kufungua njia za kibinadamu unaendelea kushika kasi, huku mashinikizo kwa Israel na Hamas yakiongezeka ili kuokoa maisha ya raia na kuruhusu upatikanaji wa misaada muhimu.