Israel yasema mauaji ya maafisa wa afya Gaza lilikuwa kosa
21 Aprili 2025Ripoti ya jeshi la Israel kuhusu mauaji ya wafanyakazi 15 wa kutoa huduma za dharura Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, imekiri jana Jumapili kwamba makosa yalisababisha vifo vyao na kwamba kamanda aliyesimamia operesheni hiyo katika uwanja wa vita atafutwa kazi.
Meja Jenerali wa akiba Yoav Har-Even, aliyeongoza uchunguzi huo, amekubali kwamba vikosi vya Israel vilifanya kosa.
Uchunguzi huo hata hivyo haukupata ushahidi wowote wa ufyetuaji risasi kiholela uliofanywa na vikosi vya Israel na kushikilia msimamo kwamba baadhi ya waliouliwa walikuwa wanamgambo.
Shirika la Hilal nyekundu la Palestina limekanusha na kuikosoa ripoti hiyo kwamba imejaa uongo.
Madaktari na wafanyakazi wengine wa uokoaji waliuwawa wakati walipokwenda kutoa huduma karibu na mji wa Rafah kusini mwa mji wa Gaza mnamo Machi 23, siku kadhaa baada ya Israel kuanzisha tena operesheni yake huko Gaza.