Israel yasema imewaua magaidi huko Ukingo wa Magharibi
2 Februari 2025Jeshi la Israel limesema leo kwamba limewaua "magaidi kadhaa" katika mashambulio matatu ya anga yaliyofanyika hapo jana katika eneo inalolikalia kimabavu la Ukingo wa Magharibi. Mashuhuda katika eneo hilo wanasema operesheni hiyo kubwa iliendelea hadi majira ya asubuhi hii leo.
Taarifa ya jeshi la Israel imeongeza kuwa imefanya mashambulizi mengine mawili huko Jenin na kusema kwamba imeisambaratisha moja ya kambi ya kigaidi katika eneo la Qabatiya na kwamba mmoja wa waliouawa aliachiliwa kutoka jela ya Israel mwaka 2023 katika awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano kwenye Ukanda wa Gaza.
Soma pia: Machozi na shangwe kwa Wapalestina walioachiwa Ukingo wa Magharibi
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kuanza mazungumzo ya awamu ya pili ya kusitisha mapigano huko mjini Washington siku ya Jumatatu. Hayo ni kwa mujibu wa ofisi yake baada ya kukamilika kwa duru ya nne ya kubadilishana wafungwa.
Tarehe rasmi ya mazungumzo yanayohusisha wapatanishi na wajumbe kutoka Hamas na Israel bado haijawekwa wazi huku awamu ya kwanza siku 42 ikitarajiwa kukamilika mwezi ujao.