Israel yaonya juu ya mkururo mpya wa makombora kutoka Iran
16 Juni 2025Jeshi la Israel limeonya leo juu ya mkururo mpya wa mashambulizi ya makombora kutokea Iran, huku waandishi wa habari wa shirika la AFP wakiripoti milipuko mikubwa mjini Jerusalem na moto nje ya mji wa pwani wa Haifa.
Tangu jana Jumapili, Israel ilifanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran wakati Tehran nayo ikijibu kwa makombora mapya huku pande zote mbili zikitishia kufanya uharibifu zaidi.
Israel imewaelekeza raia wake kuhamia kwenye maeneo salama ya kujikinga, wakati Iran ikisema kuwa itafungua misikiti, vituo vya treni za metro na shule ili kutumika kama maeneo ya kujihifadhi.
Navyo vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa, Mkuu wa ujasusi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi Mohammed Kazemi, ni miongoni mwa majenerali watatu waliuawa katika mashambulizi ya Israel jana Jumapili.
Wizara ya afya ya Iran pia imeripoti vifo vya watu 224 na wengine zaidi ya 1,200 kujeruhiwa. Kwa upande wa Israel, mamlaka zimeripoti vifo vya watu 13 tangu Iran ilipochukua hatua ya kujibu mashambulizi.