Israel yamuua kiongozi mwengine wa Hamas
28 Mei 2025Mohammed Sinwar ni mdogo wake aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo la Hamas Yahya Sinwar aliyeuwawa na Israel katika mapambano mjini Gaza mnamo Oktoba 16 mwaka jana, muda mfupi baada ya kuteuliwa kuchukua nafasi ya Ismail Haniyeh kiongozi wa Hamas pia aliyeuwawa mjini Tehran. Akizungumza bungeni Netanyahu aliongeza jina la Mohammad Sinwar katika orodha ya viongozi wa Hamas waliouwawa na Israel.
"Ndani ya siku 600 ya vita, tumebadilisha muonekano wa Mashariki ya Kati. Tumewaondoa magaidi katika eneo letu, kuingia katika ukanda wa Gaza kwa nguvu, kuwafurusha maelfu ya magaidi, kwa kumuua Mohammed] Deif, [Ismael] Haniyeh, Yahya Sinwar, na Mohammed Sinwar," alisema Netanyahu.
Netanyahu aapa kuwarudisha nyumbani mateka wote
Haya yanaripotiwa wakati wizara ya afya ya Gaza ikitangaza kuwa, raia mmoja wa kipalestina ameuwawa na wengine 48 wakijeruhiwa baada ya risasi kufyatuliwa kwa makundi ya watu, waliokuwa wamekusayika kupokea msaada kutoka kwa wakfu wa Israel wa GHF.
Hali ya msukumano ilijitokeza baada ya baadhi ya wapalestina kuvunja uzio karibu na kituo hicho cha kutoa msaada. Haikuwa wazi ni kina nani hasa waliofyetua risasi kati ya vikosi vya serikali ya Israel au makundi mengine yasiojulikana. Israel imeapa kudhibiti eneo la Gaza na kupambana na wanamgambo wa Hamas, hadi watakapowarejesha nyumbani mateka 58 wa Israel, ambao bado inawashikilia tangu waliposhambulia Kusini mwa Israel hatua iliyosababisha mgogoro unaoshuhudiwa sasa.
GHF yasitisha kwa muda utoaji wa misaada ya kiutu Gaza
Wakati uo huo wakfu wa GHF umesema usambazaji wa misaada mjini Gaza, umesimamishwa kwa muda kutokana na sintofahamu hiyo iliyojitokeza awali na kusema kwamba inajitahidi, kusuluhisha tatizo lililojitokeza ili kuhakikisha usalama wakati wa usambazaji wa misaada hiyo.
Kwengineko wafanyakazi takriban 120 wa mashirika ya misaada katika Ukanda wa Gaza, waliandamana hadi katika ofisi ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani mjini Berlin, wakidai kuwa Israel ni lazima iheshimu sheria ya kimataifa kuhusu misaada. Waandaaji wa maandamano hayo pia wametoa wito wa kupelekwa kwa malori zaidi ya misaada kwa watu wa Gaza na kusitishwa mashambulizi dhidi ya vituo vya afya.
Mamia ya Wapalestina wavamia vituo vya msaada Gaza licha ya hofu ya ukaguzi wa kibayometriki
Ujerumani imekuwa muungaji mkono mkubwa wa Israel tangu ilipoanzisha mashambulizi yake dhidi ya Hamas Oktoba 7 2023 lakini serikali ya kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, wiki hii imeikosoa vikali Israel kwa namna inavyoendesha vita vyake katika Ukanda wa Gaza. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Johann Wadephul aliyeko ziarani mjini Washington Marekani kukutana na mwenzake wa taifa hilo Marco Rubio awali alisema Ujerumani huenda ikaacha kuiuzia silaha Israel iwapo taifa hilo, litakiuka sheria ya kimataifa ya kibinaadamu ambayo Ujerumani inaiheshimu.
afp,reuters,ap