Israel yakosolewa kwa kuzuia misaada ya kiutu kuingia Gaza
3 Machi 2025Hatua ya Israel inafuatia baada ya kundi la Hamas kukataa kurefushwa kwa mkataba wa kusitisha mapigano uliomalizika Jumamosi.
Wapatanishi wa mzozo huo mataifa ya Misiri na Qatar wameituhumu Israel kukiuka sheria ya kimataifa ya misaada ya kiutu na kushambulia kwa maneno kuwa inatumia njaa kama silaha ya vita.
Kwa upande wake Mratibu wa Misaada ya Kiutu wa Umoja wa Mataifa Fletcher amesema uamuzi huo wa Israel "unatia mashaka" huku Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema utawala mjini Tel Aviv unao wajibu wa kuhakikisha misaada ya kiutu inaingia Gaza.
Israel ilitangaza jana Jumapili kusitisha upelekwaji chakula na mahitaji mengine kwenye Ukanda wa Gaza hadi kundi la Hamas litaporidhia kurefusha makubaliano ya sasa ya kusitisha vita.
Kundi hilo linalotawala Gaza limekataa mpango huo na badala linaitaka Israel kurudi kwenye meza ya mazungumzo na kujadili awamu ya pili ya kusitisha vita.