Israel yakanusha tuhuma za mauaji ya kimbari ukanda wa Gaza
2 Septemba 2025Wapalestina 31 wameuawa kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel katika ukanda wa Gaza huku jeshi la nchi hiyo likiendelea na operesheni kubwa katika mji mkuu wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa maafisa wa afya, zaidi ya nusu ya waliopoteza maisha ni wanawake na watoto, ikiwemo watu 13 waliouawa katika mashambulizi makubwa yaliyofanyika Gaza City.
Israel imetangaza Gaza City kuwa eneo rasmi la mapigano, hali iliyosababisha mashambulizi ya mara kwa mara kusikika katika maeneo mbalimbali ya mji huo.
Wataalamu wa kimataifa wa masuala ya mauaji ya kimbari wameituhumu Israel kwa mauaji ya kimbari, tuhuma ambazo serikali ya Jerusalem imekanusha vikali, ikisisitiza kuwa operesheni zake zinalenga kuangamiza miundombinu ya Hamas.
Wataalamu hao wamesema idadi kubwa ya vifo, hasa miongoni mwa wanawake na watoto, inaashiria ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, jumla ya Wapalestina 63,557 wameuawa tangu kuanza kwa vita hivyo, huku wengine 160,660 wakijeruhiwa. Ingawa wizara hiyo haitofautishi kati ya raia na wapiganaji katika takwimu zake, inasisitiza kuwa wanawake na watoto wanawakilisha zaidi ya nusu ya waliopoteza maisha.