Israel yakabiliwa na shinikizo kufuatia vita vya Gaza
30 Aprili 2025Siku ya Jumanne, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu Amnesty International liliituhumu Israel kufanya "mauaji ya halaiki" mbele ya macho ya ulimwengu. Vilevile kesi dhidi ya Israel na dhima yake kwa hali mbaya ya kiutu huko Gaza iliendelea kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICJ.
Mbali na ripoti hiyo ya Amnesty na kesi inayoendelea kwenye mahakama hiyo ya ICJ, Israel ilikabiliwa pia na shinikizo la ziada kutoka kwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za muungano wa BRICS walioitaka Israel "kuviondoa kabisa" vikosi vyake katika Ukanda wa Gaza , huku wakisisitiza kuwa kizuizi cha misaada kwa zaidi ya siku 50 katika eneo hilo ni kitendo "kisichokubalika."
Israel yaadhimisha siku ya wahanga wa ugaidi
Israel iliadhimisha Jumanne siku ya kumbukumbu ya wanajeshi na wahanga wa vitendo vya ugaidi ambapo kwa mwaka wa pili mtawalia, siku hiyo imeadhimishwa chini ya kiwingu cha vita vya Gaza ambapo jeshi la nchi hiyo bado linalaumiwa kwa kushindwa kuzuia shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023.
Tangu mwaka 1860, jumla ya askari na wapiganaji wa kiyahudi wapatao 25,420 wameuawa, hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya Ulinzi. Takwimu hizi zilianza kuorodheshwa wakati wa uhamiaji wa Wayahudi katika eneo la Israel ya sasa, ikiwa ni muda mrefu kabla ya serikali kuanzishwa rasmi mnamo mwaka 1948.
Soma pia: Israel yaipuuza ripoti ya Amnesty International kuhusu mauaji ya Gaza
Rais Isaac Herzog aliwatolea wito watu wa Israel kushikamana wakati huu kukishuhudiwa migawanyiko ya kisiasa huku akitaka vyombo vya usalama hutohusishwa na malumbano hayo:
" Tusitengane wenyewe kwa wenyewe. Tusiharibu nyumba yetu. Wito wangu ni kuiondoa IDF, Shin Bet, Mossad, Polisi, na huduma zote za usalama kwenye migogoro yote. Kwa sasa, tuwaimarishe watetezi wa ardhi yetu takatifu kama tunavyoagizwa na mafundisho."
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres jana amewatolea wito viongozi wa dunia kuonyesha "ujasiri wa kisiasa" ili kuwezesha suluhu la mataifa mawili katika mzozo kati ya Israel na Palestina huku akisema kuwa miezi 18 ya vita huko Gaza imepelekea hali ya kibinaadamu kuwa mbaya zaidi.