Israel yaomba kikao Baraza la Usalama kujadili mateka
5 Agosti 2025Ikiungwa mkono na Marekani na Panama, Israel iliamua kuitisha siku ya Jumanne (Agosti 5) kikao cha dharura ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzungumzia jaala ya mateka wake walioko Ukanda wa Gaza.
"Dunia inapaswa kukomesha dhana ya utekaji nyara raia, na suala hili lazima liwe kiini cha mazungumzo ya kilimwengu kwa sasa," alisema waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Israel, ambaye alithibitisha kuhudhuria kikao hicho jijini New York.
Kati ya mateka 251 waliochukuliwa wakati wa uvamizi wa wanamgambo wa Kipalestina dhidi ya eneo la kusini mwa Israel mnamo Oktoba 2023, wanaoendelea kushikiliwa kwenye Ukanda wa Gaza ni 49, wakiwemo 27 ambao jeshi la Israel linasema wameshakufa.
Israel na washirika wake hao waliitisha kikao hicho baada ya makundi ya wanamgambo wa Kipalestina kusambaza wiki iliyopita video tatu zinazowaonesha mateka wawili, Rom Braslavski na Evyatar David, wakiwa dhaifu na waliokondeana, na kusababisha ghadhabu na mshituko mkubwa ndani ya Israel.
Netanyahu aendelea kukosolewa
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema waliliomba Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu kuwapatia chakula na madawa mateka hao.
Tawi la kijeshi la Hamas lilisema lipo tayari kuruhusu misaada kuwafikia mateka hao lakini kwa mabadilishano ya kufunguliwa kwa njia za misaada kote Ukanda wa Gaza, ambako wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameonya baa la njaa linanukia.
Serikali ya Netanyahu imekuwa ikishutumiwa vikali na ndugu wa mateka hao na wakosoaji wengine kwa kushindwa kuchukuwa hatua za kutosha kuwaokowa.
"Netanyahu anaipeleka Israel na mateka kwenye maangamizi. Kwa miezi 22, umma umekuwa ukidanganywa kwamba shinikizo la kijeshi na mapigano makali yangewarejesha mateka nyumbani. Lakini ukweli lazima usemwe: kutanuwa vita kunahatarisha maisha ya mateka hao, ambao tayari wapo kwenye hatari ya kifo." Ilisema taarifa iliyotolewa siku ya Jumatatu (Agosti 4) na Jumuiya ya Familia za Mateka na Waliopotea.
Netanyahu amejikuta akikabiliwa na shinikizo kubwa la ndani na nje ya nchi yake linalomtaka kuwarejesha salama mateka waliobakia mikononi mwa wapiganaji wa Kipalestina ndani ya Gaza na wakati huo huo kuruhusu misaada zaidi ya kibinaadamu kwa watu wanaokufa na njaa kwenye Ukanda huo.
Mkakati wa ushindi wa Israel
Netanyahu aliahidi siku ya Jumatatu kwamba angelitowa maelekezo rasmi ya mpango wake wa kivita kwenye Ukanda wa Gaza, ambapo aliliambia baraza la mawaziri kwamba baadaye wiki hii angeliamuru jeshi jinsi ya kile alichokiita "kufikia malengo yote matatu ya vita" waliyoyaweka.
Netanyahualiyataja malengo hayo kuwa ni "kumshinda adui, kuwaachia huru mateka na ahadi kwamba Gaza haitokuwa tena kitisho kwa Israel."
Vyombo vya habari nchini Israel vimewanukuu maafisa kwenye ofisi ya Netanyahu wakisema mkakati huo mpya utakuwa ni kuukalia tena kimabavu Ukanda mzima wa Gaza, likiwemo eneo la Gaza City ambako jeshi linaamini kuwa mateka wa Israel ndiko wanakoshikiliwa.
Baraza hilo la mawaziri lilitarajiwa kukutana baadaye siku ya Jumanne kuuidhinisha mpango huo, kwa mujibu wa vyanzo serikalini.
Ingawa hakukuwa na uthibitisho rasmi juu ya azma hiyo ya Netanyahu, lakini wizara ya mambo ya kigeni ya Mamlaka ya Palestina iliulaani ule uliouita "mpango uliovujishwa" na kuitolea wito jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kuondosha uwezekano wa ukaliaji mwengine wowote wa kijeshi ndani ya Gaza.
AFP, Reuters