Israel yaishambulia Sanaa
6 Mei 2025Televisheni ya Al-Masirah inayoendeshwa na Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran, imetangaza leo kuwa shambulizi hilo linafuatia mashambulizi ya anga ya Israel katika bandari ya Hodeidah nchini Yemen Jumatatu, ikiwa ni katika kujibu shambulizi la kombora lililorushwa na Wahouthi na kuangukia karibu na uwanja mkuu wa ndege wa Israel.
Aidha, watu walioshuhudia wameripoti kuhusu mashambulizi manne ya Israel. Mvutano umeongezeka kati ya Israel na waasi wa Kihouthi wa Yemen, kutokana na waasi hao kuendeleza mashambulizi ya kujibu operesheni za Israel katika Ukanda wa Gaza.
Netanyahu aapa kulipiza kisasi
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu aliapa kulipiza kisasi baada ya kombora lililorushwa na Wahouthi kuangukia karibu na Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion, hatua iliyosababisha mashirika ya ndege ya Ulaya na Marekani kusitisha safari zake.
Israel imefanya mashambulizi hayo baada ya jeshi lake kuwataka watu kuondoka haraka katika uwanja wa ndege wa kimataifa kwenye mji mkuu Sanaa, ili kuepuka kujiweka katika hatari, kutokana na shambulizi la kombora karibu na uwanja wa ndege wa Tel Aviv. Awali, katika chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii wa X, msemaji wa jeshi la Israel aliwataka watu kupeana taarifa katika eneo hilo kuhusu ''tahadhari ya dharura.''
Wakati huo huo, Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich amesema kuwa ushindi wa nchi yake katika vita vyake dhidi ya kundi la wanamgambo wa Hamas inamaanisha kuwa Ukanda wa Gaza "utaangamizwa kabisa".
''Gaza itaangamizwa kabisa, kwa sababu ina miundombinu ya kigaidi, juu na chini ya ardhi. Raia watapelekwa eneo la kusini, kati ya miji ya kusini ya Khan Yunis na Rafah, kwenye eneo la kibinaadamu lisilokuwa na wapiganaji wa Hamas wala ugaidi. Kuanzia hapo wataanza kuondoka kwa kwa idadi kubwa kwenda kwenye nchi za tatu. Hili litabadilisha uhalisia, historia ya taifa la Israel kwa miongo kadhaa ijayo,'' alisisitiza Smotrich.
Smotrich, ameyasema hayo kwenye mkutano ambao ulikuwa unajadili suala la makaazi ya Walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Waziri huyo anayeishi katika makaazi ya Ukingo wa Magharibi, pia ameelezea matumaini yake kwamba eneo hilo litachukuliwa rasmi wakati wa muhula wa serikali ya sasa, ambao unaweza kudumu hadi mwishoni mwa mwaka ujao.
(AFP, AP, DPA, Reuters)