Israel yaishambulia Qatar ikiwalenga Hamas
9 Septemba 2025Kituo cha televisheni cha Al-Jazeera nchini Qatar kilionesha video inayoonesha moshi mkubwa ukizuka kwenye eneo ambalo kimesema ni karibu na makao rasmi ya mabalozi wa kigeni na zilipo pia ofisi za viongozi wa Hamas wanaoishi uhamishoni nchini humo.
Sauti ya miripuko mitano, kwa mujibu wa Al-Jazeera, ilisikika kwenye eneo kubwa la mji mkuu wa Qatar, Doha.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel ilisema kuwa mashambulizi hayo yamefanywa na Israel pekee bila ya kushirikiana na mtu mwengine.
Afisa mmoja wa jeshi aliliambia shirika la habari la AP kwamba mashambulizi hayo majira ya jioni ya Jumanne (Septemba 9) yalikuwa ni kwa ajili ya kuuangamiza uongozi wa kundi la Hamas, akiwataja Khaled Al-Hayya na Zaher Jawarin, ambao Tel Aviv inawatuhumu kuhusika na uvamizi wa Oktoba 2023.
Hamas yenyewe ilithibitisha kufanyika mashambulizi hayo, ikisema viongozi wake walikuwa wanakutana kujadili pendekezo la kusitisha mapigano lililotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani, ambalo tangu hapo walishalikubali.
Hata hivyo, kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina lilisema viongozi wake wote walikuwa wamenusurika kwenye mashambulizi hayo.
Qatar yalaani
Kwa upande wake, Qatar, ambayo pamoja na Marekani na Misri, ni mmoja wa wapatanishi wa mzozo huo wa Mashariki ya Kati na ambayo imekuwa mwenyeji wa viongozi kadhaa wa Hamas, imeyalaani mashambulizi hayo iliyoyaita "uvunjaji mkubwa wa sheria zote za kimataifa na yaliyofanywa na watu waoga."
Katika taarifa yake, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya taifa hilo la Kiarabu, Majid al-Ansar, alisema uchunguzi wa kina ulikuwa umeanza juu ya mashambulizi hayo na taarifa kamili ingelitolewa baada ya uchunguzi huo kukamilika.
Saudi Arabia, Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu ziliyalaani mashambulizi hayo ya Israel, ambapo Tehran iliyaita kuwa ni "muendelezo wa tabia ya Israel dhidi ya uhuru na heshima ya mataifa mengine", huku Imarat ikisema ilikuwa inasimama upande wa ndugu zao wa Qatar mbele ya kile ilichokiita "tukio la kihaini."
Marekani haikutowa kauli yoyote kuhusu mashambulizi hayo, lakini ripoti zinasema Israel ilikuwa imeijuilisha Washington kabla ya kuyafanya.
Ubalozi wa Marekani nchini Qatar ulitoa tangazo la kuwataka raia wake nchini Qatar kujificha kwenye maeneo salama.
Awali, Trump alikuwa amewatishia Hamas kwamba kutokukubaliana na pendekezo lake la amani kungekuwa na matokeo mabaya kwao, kauli ambayo wengine wanasema inaashiria rais huyo wa Marekani na muungaji mkono mkubwa wa Israel alikuwa anakijuwa kilichokuwa kinapangwa.