Jeshi la Israel lafanya mashambulizi Lebanon
28 Machi 2025Kulingana na shirika la habari la Associated Press, sauti ya mlipuko mkubwa imesikika katika mji mkuu Beirut na moshi umeshuhudiwa ukitokea kwenye eneo ambalo jeshi la Israel liliapa kulilenga.
Mapema Ijumaa jeshi hilo lilitoa onyo kwa wakaazi likiwataka waondoke haraka katika baadhi ya maeneo yaliyo nje kidogo mwa mji huo mkuu na liliapa kwamba lingelipa kisasi kutokana na mashambulizi yaliyofanywa kaskazini mwa Israel kutoka Lebanon. Maeneo hayo yaliyoshambuliwa yanafahamika kuwa ngome kuu ya kundi la Hezbollah.
Soma zaidi: Lebabon: Israel haitaki kusitisha vita
Kundi hilo hata hivyo limekanusha kuwa halikuhusika na mashambulizi hayo na limesema Israel inatafuta sababu ya kuendelea kuishambulia Beirut.
Rais wa Lebanon Joseph Aoun ame yalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya taifa lake na kile alichokiita jaribio la kurejesha upya vurugu katika nchi hiyo ndogo. Ameitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wake na wanahabari akiwa sambamba na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Paris.
Lebanon yachunguza kubaini waliohusika kuirushia Israel makombora
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa wa Lebanon Nawaf Salam amelitaka jeshi nchi yake lifanye uchunguzi mara moja ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika kurusha makombora kuelekea Israel.
Naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema hakuna kitu chochote cha kuhalalisha mashambulizi ya Ijumaa ya Israel dhidi ya Hezbollah na kwamba atawasiliana kwa njia ya simu na Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ndani ya saa 48 zijazo ili kuyajadili mashambulizi hayo.
Israel na Hezbollah walikubaliana kusitisha vita mwezi Novemba mwaka uliopita. Makubaliano hayo yalilitaka kundi la Hezbollah kuondoa silaha zake kusini mwa Lebanon, vikosi vya Israel viondoke nchini humo na jeshi la Lebanon liwapeleke wanajeshi wake katika eneo hilo. Tangu wakati huo kumekuwa na kushutumiana kwa pande zote za mzozo kuwa zinakiuka makubaliano ya kuweka chini silaha.