Israel yaishambulia Iran
13 Juni 2025Kwa mujibu wa televisheni ya serikali ya Iran, mkuu wa Kikosi Maalum cha Walinzi Mapinduzi, Meja Hossein Salami, ni miongoni mwa waliouawa.
Wengine waliouawa ni mbunge na mwanasayansi wa nyuklia, Feyyudin Abbasi, na mkuu wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Azzad mjini Tehran, Mohammad Mehdi Tehranchi.
Soma zaidi: Israel yafanya mashambulizi katika mji mkuu wa Iran, Tehran
Kumeripotiwa pia vifo vya raia, wakiwemo watoto.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amedai kuwa mashambulizi hayo yalidhamiria kuizuwia Iran kuendeleza programu yake ya nyuklia ambayo amesema ni hatari kwa usalama wa Israel.
Miongoni mwa miji iliyoshambuliwa ni mji mkuu Tehran, Qom na Tebriz.
Wizara ya usafirishaji ya Israel imelifunga anga la nchi hiyo, huku jeshi likisema linatazamia mashambulizi kutoka Iran wakati wowote.
Iran nayo imelifunga anga lake, sawa na taifa jirani la Iraq.
Marekani yajitenga na kuhusika
Marekani imesema ilijulishwa kabla na Israel juu ya dhamira yake ya kufanya mashambulizi hayo, lakini imekanusha kuhusika kwa namna yoyote kwenye operesheni hiyo, ambayo Netanyahu amesema itaendelea kadiri itakavyohitajika.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, ameionya Iran dhidi ya kuchukuwa hatua yoyote kwa wanajeshi, maslahi na maafisa wa Marekani kwenye eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati.
Soma zaidi:Iran yazishutumu Israel, Marekani kwa anguko la Assad
Tehran ilishasema tangu awali kwamba endapo mashambulizi kama hayo yangelifanywa dhidi yake, ingeliwachukulia wote walioshirikiana na Israel kuwa shabaha ya kulipiziwa kisasi.