Israel yailaumu Lebanon kwa kuishambulia, yajibu mapigo
28 Machi 2025Kulingana na taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa Ijumaa asubuhi, kombora moja lililoelekezwa Galilaya lilizuiwa wakati jingine lilianguka ndani ya eneo la Lebanon.
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema serikali ya Lebanon inawajibika moja kwa moja kwa mashambulizi yoyote yanayoelekezwa katika eneo la Galilaya. Shambulio hilo dhidi ya Israel limefanywa siku moja baada ya Lebanon kulilaumu jeshi la Israel kwa kufanya mashambulizi yaliyosababisha mauaji ya watu sita kusini mwa nchi hiyo.
Hata hivyo Israel imejibu ikisema kuwa mashambulizi yake yaliilenga miundombinu ya kundi la Hezbollah. Kundi hilo kupitia jukwaa la telegram limesema linaheshimu makubaliano ya kusitisha vita na halihusiki na makombora yaliyorushwa Kaskazini mwa Israel.
Licha ya Hezbollah kukanusha kuhusika na mashambulizi hayo, muda mfupi uliopita, jeshi la Israel limetangaza kuwa limeanza kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la Hezbollah kusini mwa Lebanon. Taarifa ya jeshi hilo imesema maelezo zaidi kuhusu operesheni hiyo yatatolewa baadaye.
Juhudi za kuokoa makubaliano ya kusitisha vita zaendelea
Wakati huo huo, vyanzo kutoka Palestina vimesema mazungumzo yanaendelea kati ya kundi la wanamgambo wa Hamas na wasuluhishi kutoka Misri na Qatar ili kujaribu kufufua makubaliano ya kusitisha vita kwenye Ukanda wa Gaza na kuwaachilia huru mateka.
Vyanzo hivyo ambavyo vimezungumza kwa sharti la kutotajwa jina vimeeleza kuwa mazungumzo hayo yamejikita katika kuangalia uwezekano wa kutekeleza usitishaji wa vita wakati wa sikukuu ya Eid al Fitr na katika msimu wa sikukuu ya Wayahudi. Majadiliano hayo yanadhamiria pia kuhakikisha kuwa misaada ya kiutu inaingizwa kwenye Ukanda wa Gaza.
Mazungumzo ya usuluhishi kati ya kundi la Hamas na Israel yanayosimamiwa na Misri, Marekani na Qatar yamekwama kwa wiki kadhaa baada ya kwisha kwa muda wa awamu ya kwanza ya kusitisha vita Januari 19.
Yanafanyika ikiwa ni siku moja tangu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atishie kuyatwaa maeneo ya Gaza kama wanamgambo wa Hamas hawatawaachilia mateka. Wanamgambo hao walijibu wakionya kuwa kama Israel isipoacha kufanya mashambulizi Gaza, mateka hao watarejeshwa nchini humo wakiwa kwenye majeneza.