Israel yaidhinisha mashambulizi mapya Gaza
13 Agosti 2025Mkuu wa Majeshi ya Israel, Luteni Jenerali Eyal Zamir, ameidhinisha mpango wa mashambulizi Gaza, likilenga tena Jiji la Gaza ambako maelfu wamekimbilia. Hayo yanajiri wakati Hamas ikianza mazungumzo ya kusitisha mapigano.
Jeshi la Israeli limesema Jumatano kwamba Mkuu wa Majeshi, Luteni Jenerali Eyal Zamir, ameidhinisha muundo mkuu wa mpango wa mashambulizi katika Ukanda wa Gaza.
Lengo la Israel: Kudhibiti Tena Jiji la Gaza
Israel imesema itazindua mashambulizi mapya na kuchukua tena udhibiti wa Jiji la Gaza, ambalo ililiteka muda mfupi baada ya kuzuka kwa vita mwezi Oktoba 2023, kabla ya kujiondoa.
Serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu haijatoa ratiba kamili ya wakati ambapo majeshi ya Israeli yataingia katika jiji kubwa zaidi la eneo hilo, ambako maelfu ya watu wamekimbilia kutafuta hifadhi baada ya mashambulizi ya awali.
Ukosoaji wa Kimataifa: New Zealand Yatoa Kauli Kali
Lakini wakati Israel ikiendelea na mipango hiyo, kiongozi wa New Zealand Christopher Luxon, amemtuhumu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuwa amepoteza mwelekeo na kwamba vita vyake huko Gaza vimepita kiasi.
"Nadhani amepoteza mwelekeo. Na nadhani kile tulichokiona usiku wa kuamkia leo, shambulio dhidi ya Jiji la Gaza, ni jambo lisilokubalika kabisa kabisa. Na hicho ndicho tumekuwa tukikisema kama jumuiya ya kimataifa kwa muda mrefu sasa. Yeye hasikilizi jumuiya ya kimataifa, na hilo halikubaliki."
Hatari ya Njaa na Ukosoaji wa Kimataifa
Wakati hayo yakijiri, Wataalamu wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wameonya kuhusu njaa kubwa inayozidi kuenea katika eneo hilo, ambako Israel imezuia kwa kiwango kikubwa kuingia kwa misaada ya kibinadamu.
Israel imekumbwa na ukosoaji mkubwakuhusu vita hivyo, ambavyo vilichochewa na shambulio la kundi la wanamgambo wa Kipalestina, Hamas, dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023,
Mazungumzo ya Kusitisha Mapigano: Hamas Yawasili Cairo
Kundi hilo ambalo Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya huliita kuwa la kigaidi, bado linashikilia mateka 50.
Mnamo Jumanne, Netanyahu, alidokeza kwamba juhudi za kusitisha mapigano huko Gaza sasa zimeelekezwa kwenye makubaliano ya jumla yatakayowezesha kuachiliwa kwa mateka wote waliobaki kwa pamoja, wala si kwa awamu.
Habari kuhusu jeshi kuidhinisha mpango wa operesheni Gaza imejiri saa chache baada ya Hamas kusema kuwa ujumbe wake wa ngazi ya juu umefika mjini Cairo kwa ajili ya 'mazungumzo ya awali' na maafisa wa Misri kuhusu kusitisha mapigano kwa muda.
Shinikizo kwa Hamas na Ukosoaji wa Mpango Mpya
Mpango huo wa kutanua vita hadi maeneo ambako takriban wakaazi milioni 2 wamekimbilia kutafuta hifadhi, umekosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa ikiwemo Ujerumani, na huenda unalenga kuongeza shinikizo kwa Hamas ili kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano."
(APE,AFPE,RTRE)