Israel yaendesha mauaji ya kimbari Gaza -mashirika ya haki
29 Julai 2025Madai hayo yaliyotolewa na mashirika ya B'Tselem na Madaktari kwa Ajili ya Haki za Binaadamu yanaongeza sauti za ukosoaji dhidi ya matendo ya jeshi la Israel kwenye Ukanda huo.
Hii ni mara ya kwanza kwa mashirika ya ndani ya Israel kuihusisha nchi hiyo na mauaji ya kimbari.
Haya yanakuja wakati jeshi la Israel likiwauwa Wapalestina 78 kwenye maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita, akiwamo mwanamke mjamzito ambaye mtoto wake alitolewa baada ya kuuawa kwake.
Watu kadhaa kati ya waliouawa walikuwa wakisaka msaada wa chakula, ingawa Israel imetangaza kulegeza vikwazo cha kuingia msaada kwenye Ukanda huo.
Kufuatia shinikizo la kimataifa, jeshi la Israel lilitangaza kuanza kusitisha operesheni zake kwa masaa 10 kwa siku ili kuruhusu misaada kuwafikia raia kwenye maeneo ya Gaza City, Deir al-Balah na Muwasi, lakini mashirika ya misaada yanasema hatua hiyo haitoshi kukubaliana na ukosefu mkubwa wa chakula uliopo.