Israel yaendeleza mpango wa kupanua operesheni za kijeshi
21 Agosti 2025Zaidi ya askari wa akiba 60,000 wameitwa kazini na maandalizi yanaendelea katika maeneo ya Zeitoun na Jabaliya. Operesheni kamili ya kuchukua udhibiti kimabavu wa mji wa Gaza inaweza kuanza ndani ya siku chache.
Kwa mujibu wa afisa ambaye hakuwa na ruhusa ya kuzungumza na vyombo vya habari, Netanyahu anatarajiwa kutoa idhini ya mwisho kwa operesheni hiyo katika kikao cha baraza la usalama Alhamisi usiku.
Msemaji wa Jeshi la Israel, Brigedia Jenerali Effie Defrin, amesema "Tutazidisha mashambulizi dhidi ya Hamas katika Mji wa Gaza, ambao ni ngome ya kigaidi ya kijeshi na kiserikali ya kundi hilo la kigaidi. Tutashambulia kwa nguvu zaidi miundombinu ya kigaidi ya angani na ardhini na kukatisha utegemezi wa wakazi kwa Hamas."
Jeshi laagiza wahudumu wa afya kufanya maandalizi
Jeshi la Israel limethibitisha kuwa limewafahamisha wahudumu wa afya na mashirika ya misaada waanze kupanga mipango ya kuhamisha raia na vifaa muhimu kutoka hospitali za kaskazini kuelekea kusini mwa Gaza na kwamba linafanya marekebisho ya miundombinu ya hospitali kusini mwa Gaza ili kuwapokea majeruhi.
Hata hivyo, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA Philippe Lazzarini ameonya kuwa watoto waliodhoofika kwa njaa hawawezi kuhimili tena uhamisho, akisema bila mpango wa dharura, wengi wao watakufa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amerudia wito wake wa kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka wote bila masharti.
"Ni muhimu sana kufikia usitishaji wa mapigano mara moja huko Gaza ili kuepusha vifo na uharibifu mkubwa ambao mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Mji wa Gaza yatawafika watu." alisema Guterres.
Huku haya yakiarifiwa kumekuwa na maandamano katika miji ya Gaza na Tel Aviv kupinga uhamishaji wa lazima na kuomba amani na huko Israel, huku familia za mateka waliobaki Gaza wakilaani operesheni hiyo wakisema inahatarisha maisha ya mateka walio hai.