Israel yadungua maroketi matatu yaliyorushwa kutoka Lebanon
22 Machi 2025Jeshi la Israel limesema leo Jumamosi kwamba limeyadungua maroketi matatu yaliyorushwa kutoka nchini Lebanon na yaliyokuwa yamelenga kushambulia eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Sauti za ving'ora vya tahadhari zilisikika katika mji wa Metula, lakini hapakuwa na ripoti za uharibifu au majeruhi. Tangu mwezi Novemba kumekuwa na usitishwaji wa mapigano nchini Lebanon kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran.
Soma zaidi.Urusi na Ukraine zashambuliana kwa makombora usiku kucha
Chini ya masharti ya kusitisha mapigano, wanajeshi wa Israel walitakiwa kujiondoa kutoka kusini mwa Lebanon, lakini vituo vyake vitano vya kijeshi bado vimesalia karibu na eneo la mpakani mwa Lebanon na serikali ya Lebanon inaona kwamba kuendelea kuwepo kwa vituo hivyo ni ukiukwaji wa makubaliano.
Baada ya tukio hilo la leo, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema vikosi vyake vitajibu mapigo dhidi ya Lebanon.