Israel yadaiwa kuwashambulia wapalestina Ukanda wa Gaza
20 Julai 2025Mauaji hayo yametokea katika eneo la Al Sudaniya Kaskazini mwa eneo linalozingirwa katika ukanda huo wa Gaza. Waathiriwa hawakuwa na silaha zozote hii ikiwa ni kulingana na walioshuhudia kisa hicho. Miili kadhaa bado imetapakaa barabarani katika eneo hilo.
Ripoti kadhaa zimesema kwamba wapalestina hao walikuwa wanasubiri malori kadhaa ya misaada karibu na eneo la mpakani mwa Israel kabla ya kushambuliwa. Israel hadi sasa haijasema lolote kuhusiana na kisa hiki.
Watu 26 wauawa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel
Wakati hayo yakiarifiwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anaugua kutokana na kile ofisi yake imesema kuwa athari ya sumu itokanayo na chakula. Netanyahu mwenye umri wa miaka 75 alizidiwa usiku wa kuamkia leo na baadae aligundulika kuwa na uvimbe kwenye utumbo mdogo na kukosa maji mwilini. Kwa sasa anapatiwa matibabu nyumbani kwake.
Ofisi yake imesema atabakia nyumbani kwa siku tatu na majukumu yake yote ya kiofisi atayafanyia huko. Netanyahu aliwahi kuwekewa kifaa cha kusawazisha mapigo ya moyo mwaka 2023, na Desemba mwaka jana alifanyiwa upasuaji wa kuondoa tezi dume baada ya kugundulika kuwa na maambukizi katika mfumo wa mkojo yaani UTI.