Israel yahamasisha askari wa akiba 60,000 kwa vita Gaza
3 Septemba 2025Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kupitia ujumbe kwa njia ya video kwa askari hao wa akiba, amesema ni lazima wamalize kile walichokianza katika ukanda wa Gaza, akieleza kuwa jukumu lao ni la msingi katika kuhakikisha usalama wa taifa.
Mapema jana, mkuu wa majeshi ya Israel Eyal Zamir, alisisitiza kwamba operesheni ya kijeshi katika ukanda wa Gaza itakuwa kali zaidi.
Zamir amesema operesheni ya kijeshi itapanuliwa kwa lengo la kuangamiza miundombinu ya Hamas na kuzuia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka Gaza.
Wakati hayo yakijiri, watoto watano wameuawa katika shambulio la hivi karibuni lililofanywa na Israel kusini wa Gaza.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina WAFA, mashambulizi hayo yametokea katika eneo la Al-Mawasi, ambalo jeshi la Israel limeliweka kama eneo salama la kibinadamu.