Israel yaamuru Wapalestina kuondoka Gaza City
6 Septemba 2025Amri hiyo imetolewa wakati jeshi hilo linatanua kampeni ya kijeshi kwenye mji huo ulio mkubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza.
Jeshi hilo hivi sasa linafanya mashambulizi makali ikiwemo kuyalenga majengo ya ghorofa ikiwa ni sehemu ya operesheni yake kubwa ya kutaka kuukamata mji huo.
Sehemu ya mji huo wenye wakaazi wanaokaribia milioni 1, inazingatiwa kuwa uwanja wa mapambano, na imetolewa amri ya watu kuondoka kabla ya kuanza mashambulizi makali zaidi ya kijeshi.
Mashirika ya misaada ya kiutu yameonya mara kadhaa kwamba kuhamishwa idadi kubwa ya watu kutoka mji huo kutazidisha madhila na balaa ambavyo tayari Wapalestina wanashuhudia tangu kuanza kwa vita vya Gaza.
Mji wa Gaza City umeorodheshwa kuwa kwenye kitisho cha kukumbwa na baa la njaa na tayari malaki ya Wapalestina wameshalazimika kuyakimbia maakazi zaidi ya mbili tangu kuanza kwa vita.
Jeshi lasema "sehemu salama" ni Al-Muwasi kusini mwa Gaza
Msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee ameandika katika ukurasa wa X kuwa Al-Muwasi kuliko na kambi iliyojengwa kwa mahema kusini mwa Ukanda wa Gaza ndio salama kwa watu kwenda.
Jeshi la Israel limeamuru kuondoka watu kutoka Gaza City kwa madai kundi la Hamas lina ngome kubwa kwenye mji huo.
Limeutaja mji huo kuwa uwanja wa vita na limewataka Wapalestina kuondoka kwa kutumia magari kupitia njia malaamu iliyotengwa bila kukumbana na kadhia ya upekuzi.
Taarifa ya jeshi, imetoa pia ramani inayoonesha eneo hilo salama linajumuisha mji wa Khan Younis. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, eneo lililotengwa kutakuwa na hospitali za muda, maji ya bomba, chakula na mahema na kwamba shughuli zote za misaada ya kibanaadamu zitaendelea kutolewa kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa.
Hata hivyo msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kiutu, Olga Cherevko amesema tangazo la maeneo hayo kuwa salamu limetolewa na Israel pekee bila kuushirikisha Umoja wa Mataifa wala mashirika mengine yanayofanya kazi ndani ya Ukanda wa Gaza.
Mara kadhaa vikosi vya Israel vimeyashambulia maeneo yanayotoa huduma za kibinaadamu katika kipindi chote tangu kuzuka kwa vita. Maeneo hayo yanajumuisha yale ambayo Israel yenyewe iliyatangaza kuwa "salama" na kuwataka Wapalestina kwenda kutafuta hifadhi.
Wakaazi wengi wa Gaza City wasema hawatoondoka
Licha ya onyo kutoka jeshi la Israel, wengi ya Wapalestina wamesema hawataondoka Gaza City.
"Wanatuamuru tuondoka kutoka mji mmoja kwenda mwengine? Tutafanya vipi na watoto wetu? Wale walio na wagonjwa, au wazee au waliojeruhiwa, watawapeleka wapi?", amesema mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Um Haitham.
Mapema siku ya Jumamosi, Israel ilitoa onyo kwa waakazi wote wa majengo marefu mawili katikati mwa Gaza City na mahema kadhaa yanayozunguka eneo hili.
Imesema ndani au pembezoni mwa eneo hilo kuna miundombinu ya kundi ya Hamas. Tahadhari hiyo inayomaanisha huenda jeshi la Israel litashambulia, imetolewa siku moja baada ya Israel kuliporomosha kwa makombora jengo moja la ghorofa katikati ya Gaza City kwa madai kwamba Hamas imekuwa ikilitumia kufanya ushushushu bila hata hivyo kutoa ushahidi.
Hayo yanajiri wakati hakuna ishara ya kupatikana mwafaka utakaomaliza vita licha ya juhudi za mataifa ya kiarabu kutafuta mkataba wa kusitisha mapigano. Mwezi uliopita, kundi la Hamas lilisema limeridhia pendekezo la kusitisha vita lililowasilishwa mezani lakini Israel hadi leo haijatoa msimamo wake.
Yenyewe imesema itaendelea na vita hadi ihakikishe mateka wake wote wamerudishwa kutoka Ukanda wa Gaza na kundi la Hamas limesambaratishwa. Pia Israel imesema hata vita vitakapomalizika itabakia kuwa na udhibiti fulani wa kijeshi kwenye ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina wapatao milioni 2.