Israel na Iran zadumisha makubaliano ya kusitisha vita
24 Juni 2025Trump, alitoa maoni yake kwa waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani kabla ya kuondoka kuelekea kwenye mkutano wa kilele wa Jumuiya ya NATO huko The Hague, nchini Uholanzi akisema amesikitishwa na nchi hizo kuendelea kushambuliana. Alipotakiwa na waandishi wa Habari kutoa maoni yake Trump alijibu:
"Wamekiuka makubaliano, lakini Israel nayo imekiuka. Israel, mara tu tulipokubaliana, walitoka na kurusha mabomu mengi zaidi kuliko nilivyowahi kuona. Kiwango kikubwa zaidi tulichowahi kushuhudia. Sifurahishwi na Israel. Unajua, ninaposema, sawa, sasa mna saa 12, hampaswi kutoka katika saa ya kwanza na kurusha kila kitu mlichonacho juu yao. Hivyo, sifurahishwi nao. Lakini pia sifurahishwi na Iran."
Soma pia: Ulimwengu wakaribisha Usitishaji vita kati Iran na Israel
Rais Donald Trump amesema Israel na Iran hawajui wanachokifanya. Hata hivyo baada ya kuzilaumu nchi hizo Rais wa Marekani amesema makubaliano ya kusimamisha vita yanaendelea kutekelezwa.
Israel imesema "inajiepusha" na mashambulizi zaidi dhidi ya Iran baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuzungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, imesema ofisi ya Netanyahu mjini Tel Aviv.
Wakati hayo yakiendelea Wairan na Waisraeli wanasherehekea amani iliyorejea kwenye maeneo yao siku ya Jumanne, licha ya ripoti kutoka pande zote mbili za ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha vita yaliyotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema aliliamuru jeshi kufanya mashambulizi mapya kwenye mji wa Tehran kujibu hatua ya Iran ya "ukiukaji wa wazi" wa makubaliano ya kusimamisha mapigano.
Iran yakanusha kuishambulia Israel
Iran kwa upande wake imekanusha kuishambulia Israel kwa makombora na imesema kwamba mashambulizi ya Israel yaliendelea kwa saa moja na nusu zaidi baada ya muda uliokusudiwa wa kuanza usitishaji wa mapigano.
Hata hivyo katika nchi zote mbili za Iran na Israel, eneo zima la Mashariki ya Kati na ulimwenguni kote, dhahiri inaonekana hisia ya uwepo wa unafuu kwamba makubaliano ya kusimamisha vita yamefikiwa, siku 12 baada ya Israel kufanya mashambulio ya kushtukiza, dhidi ya Iran na siku kadhaa baadaye Marekani ikaiunga mkono kwa kuishambulia Iran.
Waisraeli waliokwama nje ya nchi wakati wa mzozo wa nchi yao na Iran wametua katika uwanja wa ndege wa Tel Aviv leo hii Jumanne baada ya mahasimu hao kukubali kusimamisha mapigano.
Takriban Waisrael 150,000 hawakuweza kurejea nchini kwa ndege tangu Juni 13, wakati Israel ilipofunga anga yake na safari za ndege zilisitishwa baada ya Israel kuishambulia Iran.
Soma pia:Trump: Israel na Iran zimekubaliana kusitisha mapigano
Walinzi wa Mapinduzi ya Iran wamesema wamemkamata raia mmoja wa Ulaya anayetuhumiwa kufanya ujasusi kwenye maeneo "nyeti ya kijeshi" katika eneo la kusini mwa nchi hiyo.
Mtu huyo alikamatwa na vikosi vya usalama kutoka Shirika la Kijasusi la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkoa wa Hormozgan. Mtu huyo amebainika kuwa aliingia Iran kama mtalii.