Israel/Hamas kuanza tena mazungumzo ya kusitisha vita Gaza
7 Julai 2025Haya yanatokea wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akitarajiwa kukutana na rais wa Marekani Donadl Trump anayeshinikiza kuwepo kwa makubaliano ya usitishaji mapigano Gaza.
Majadiliano kuhusu vita vya Gaza yalianza jana mjini Doha, kujaribu kufikiwa makubaliano hayo, pamoja na kuachiwa mateka wanaoendelea kushikiliwa na Hamas, huku kundi hilo la wanamgambo pia likitarajia kuachiwa kwa wafungwa wa kipalestina wanaoshikiliwa Israel.
Hadi sasa lakini hapajakuwa na taarifa za kuanza rasmi mazungumzo kati ya wawakilishi wa Israel na Hamas.
Huku hayo yakiarifiwa Donald Trump kabla ya kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliyoko ziarani mjini Washington amesema, anaamini mpango wa kusitisha mapigano huenda ukafikiwa wiki ijayo.
Trump anashinikiza kufikiwa makubaliano ya kumaliza vita katika ukanda wa Gaza unaopitia hali mbaya ya kibinaadamu fuatia miaka miwili ya mashambulizi ya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas.