Israel kuwatuma wanajeshi 50,000 wa akiba Gaza
20 Agosti 2025Wizara ya Ulinzi ya Israel imethibitisha kwamba majenerali wakuu tayari wameidhinisha operesheni hiyo mpya inayolenga kuyadhibiti maeneo ya jiji la Gaza ambayo bado hayajafikiwa na jeshi la Israel, ambako inadhaniwa wapiganaji wa kundi la Hamas wapo kwa wingi na wanaendeleza shughuli za kundi hilo.
Maafisa wa kijeshi wamesema mpango huo sasa unasubiri idhini ya mwisho kabla ya kuanza kutekelezwa. Jamii ya kimataifa ina wasiwasi kuhusu raia wa kawaida kupoteza maisha yao katika eneo hilo la Gaza lenye watu wengi.
Afisa mmoja wa kijeshi aliyezungumza bila kutaka kutambulishwa amebainisha kuwa takriban askari wa akiba 50,000 wataitwa kujiunga na operesheni ya kijeshi mwezi ujao, na uwezekano wa kuongeza idadi ya askari hao wa akiba hadi takriban 120,000. Muda sahihi wa kuanza operesheni hiyo ya kijeshi katika ardhi ya Gaza bado haujawekwa wazi.
Katika Ukanda wa Gaza, Wapalestina wanajiandaa kwa wimbi jingine la mashambulio. Raia wengi waliokimbia makazi yao mara kadhaa katika muda wa miezi 22 iliyopita wanasema imani yao ni ndogo sana katika mchakato wa kusitisha mapigano.
Uamuzi wa Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz umechukuliwa huku kukiwa na mzozo kati ya Israel na Australia, baada ya nchi hiyo kuitambua Palestina kuwa ni taifa huru, hatua ambayo imezusha vita vya maneno kati ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mwenzake wa Australia, Anthony Albanese.
Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, amepuuzilia mbali shutuma za Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, aliyemwita kuwa "mwanasiasa dhaifu aliyeisaliti Israel" kwa kulitambua taifa la Palestina.
Huku hayo yakiendelea jitihada za kusitisha mapigano zinakabiliwa na hali tete wakati ambapo Israel inadai kuachiliwa kwa mateka wote 50 ambao bado wanashikiliwa katika Ukanda wa Gaza, hatua ambayo inatia shaka iwapo Israel italikubali pendekezo jipya la usitishaji vita kwa siku 60 ambalo Hamas ililikubali siku ya Jumatano. Pendekezo hilo liliwasilishwa na Qatar na Misri na linaambatana na pendekezo la Marekani ambalo Israel ilikuwa imelikubali hapo awali, kwa mujibu wa Qatar.
Pendekezo hilo linajumuisha usitishaji wa mapigano kwa siku 60, ambapo takriban nusu ya mateka wa Israel waliosalia wataachiliwa kwa kubadilishana na Israel kuwaachia wafungwa wa Kipalestina. Israel pia itaongeza kwa kiasi kikubwa uingizaji wa misaada huko Gaza katika kipindi hicho.
Pendekezo hilo linachukuliwa kuwa ni hatua ya kuelekea makubaliano mapana zaidi ya kuvimaliza vita vilivyodumu kwa takriban miaka miwili.
Vyanzo: AP/RTRE/AFP