Israel kutoondoka ukanda wa Philadelphi
27 Februari 2025Afisa wa Israel ambaye amezungumza kwa sharti la kutokutajwa jina kwa mujibu wa kanuni, amesema jeshi linahitaji kubakia katika ukanda huo wa Philadelphi, ulioko katika mpaka wa Gaza na Misri ili kuzuia biashara ya magendo ya silaha. Kulingana na makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwezi uliopita, Israel ilipaswa kuanza kuwaondoa wanajeshi wake siku ya Jumamosi, na kukamilisha shughuli hiyo ndani ya siku nane.
Aidha, akizungumza Alhamisi na viongozi wa baraza la wazee, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema jeshi la nchi hiyo litaendelea kulikalia eneo lisiloruhusiwa kuwa na shughuli zozote za kijeshi Gaza, ikiwemo ukanda wa Philadelphi.
Hamas yazungumzia kuhusu kubakia Philadelphi
''Nikiwa kama waziri wa ulinzi nilitembelea huko na kuona mahandaki, mengine yamezuiwa na mengine yanapitika kutoka Gaza kwenda upande wa Misri. Hili lina maana gani? Biashara ya magendo,'' alifafanua Katz.
Hamas imesema jaribio lolote la kuendelea kubakia kwenye njia hiyo, litakuwa ''ukiukaji wa wazi'' wa makubaliano ya kusitisha mapigano. Misri ambayo ni mpatanishi mkuu bado haijazungumzia lolote kuhusu tangazo hilo la Israel. Misri pia inapinga uwepo wa jeshi la Israel katika eneo hilo la mpaka. Jumamosi ndiyo siku ya mwisho ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israel.
Misri imesema imeharibu mahandaki yote yanayoendesha biashara za magendo kutoka upande wake miaka kadhaa iliyopita, na kuweka eneo lisiloruhusiwa kuwa na shughuli zozote za kijeshi ili kukomesha biashara hiyo.
Ama kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameuagiza ujumbe wake unaoshiriki katika mazungumzo kuondoka kuelekea Cairo Alhamisi ili kuendelea na mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza.
Ujumbe wa Israel kuelekea Cairo
Hayo yako katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya Netanyahu Alhamisi, bila ya kuwepo maelezo ya kina zaidi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar amesema ujumbe huo wa Israel utaelekea Cairo kuangalia iwapo kuna msingi wa pamoja wa majadiliano.
Wakati huo huo, Netanyahu ameahidi kufanya kazi ''bila kuchoka'' kuwarudisha nyumbani mateka wote wanaoshikiliwa Gaza, baada ya Hamas kuikabidhi mapema Alhamisi miili ya mateka wanne wa Israel. Netanyahu amesema ataendelea kuchukua hatua na kuhakikisha mateka wote wanarudi nyumbani salama.
(AFP, DPA, AP, Reuters)