Israel kuamua kuhusu mpango wa kuvitanua vita Gaza
7 Agosti 2025Serikali ya Israel itapitisha uamuzi muhimu kuhusu mpango wa kuvitanua vita katika Ukanda wa Gaza na kulikalia kikamilifu eneo hilo la Wapalestina katikati mwa mgawanyiko kuhusu mpango huo ndani ya Israel.
Netanyahu anatarajiwa kuitisha baraza lake la mawaziri la usalama siku ya Alhamisi ili kukamilisha uamuzi juu ya upanuzi wa mashambulizi hayo, vyombo vya habari vya Israel viliripoti.
Ndani ya Israel kwenyewe vyombo vya habari vimeripoti kwamba mkuu wa jeshi la Israel, Eyal Zamir ameelezea wasiwasi wake kwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakati wa mazungumzo kuhusu kuvitanua vita vya Gaza.
Zamir ametahadharisha kwamba hatua ya kuukalia ukanda wa Gaza "itakuwa ni sawa na kujiingiza katika mtego" akiwa na maana ya athari zinazoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na mateka waliosalia Gaza.