Israel itajutia hatua yake ya kuishambulia Iran
13 Juni 2025Rais Pezeshkian amesema Israel itajutia hatua yake ya kuishambulia Iran na kuyalenga maeneo muhimu vikiwemo vinu vyake vya nyuklia. Akizungumza kwenye televisheni ya taifa, rais huyo wa Iran amesisitiza kuwa taifa hilo na maafisa wake hawatobakia kimya, watajibu vikali hatua ya Israel ambayo haikuwa ya busara.
"Bila shaka taifa la Iran na maafisa wake hawatalifumbia macho hili, uhalifu huu ni lazima utajibiwa kihalali na kwa nguvu zote, Iran itaifanya adui yake kujutia hatua yake ya kipuzi," alisema Pezeshkian.
Iran yasema Israel itawajibishwa kwa kuishambulia
Kulingana na Israel, shambulizi lake limefanikiwa kuwaua maafisa zaidi wa kikosi maalum cha walinzi wa mapinduzi na imeyalenga maeneo zaidi ya 100 vikiwemo vinu vya nyuklia. Kiongozi mkuu wa taifa hilo Ayatolla Ali Khamenei, ameionya Israel kwamba hatima yake ni mbaya, kufuatia shambulizi hilo huku waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Abbas Araghchi akilielezea shambulizi hilo kama tangazo la vita.
Khamenei amethibitisha waliouwawa ni pamoja na mkuu wa kikosi maalum cha walinzi mapinduzi, Meja Hossein Salami, Mnadhimu Mkuu wa jeshi la Iran Jenerali Mohammed Bagheri, wanasayansi 6 wa nyuklia na mkuu wa chuo kikuu cha teknolojia cha Azzad mjini Tehran, Mohammad Mehdi. Takriban makamanda 20 waliangamizwa katika shambulizi hilo akiwemo mkuu wa jeshi la anga Ali Hajizadeh.
Trump aishinikiza Iran kufikia mkataba wa nyuklia
Shambulizi hilo pia limesababisha mauaji ya watu 70 huku wengine zaidi ya 329 wakiwemo wanawake na watoto wakijeruhiwa. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amedai kuwa dhamira ya hatua yake ni kuizuwia Iran kuendeleza mpango wake wa nyuklia ambao amesema ni hatari kwa usalama wa Israel. msemaji wa jeshi la Israel jenerali Effie Defrin amesema ndege 200 za kivita zilishiriki katika oeresheni hiyo.
Haya yanajiri wakati Rais wa Marekani Donald Trump akiishinikiza Iran kufikia mkataba wa nyuklia, akionya kuwa kutakuwa na vifo zaidi na uharibifu mkubwa iwapo hilo halitafanyika. Licha ya Marekani kutangaza kwamba haikuhusika na shambulizi dhidi ya Iran, imeionya nchi hiyo dhidi ya kuchukua hatua yoyote kwa wanajeshi,maslahi na maafisa wa Marekani kwenye eneo la Ghuba na Mashariki ya kati. Hata hivyo Iran imesema Washinton pia itaonya kisasi cha Tehran.
IAEA yaishtumu Iran kutozingatia wajibu wake wa kinyuklia
Nchini Iran kwenyewe maandamano yanaendelea ya kulaani shambulizi hilo huku raia wakiishinikiza nchini hiyo kulipiza kisasi na wengine wakibakia majumbani mwao wakihofia hali kuwa mbaya zaidi. Baadhi ya wachambuzi wanaliona shambulizi la leo kama chanzo cha kufuangua rasmi vita kamili kati ya mahasimu hawa wa muda mrefu Israel na Iran.
Huku hayo ya kiarifiwa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana kwa dharura kujadili shambulizi hilo huku miito ikiendelea kutolewa kwa pande hizo mbili kujizuwia na hatua zinazoweza kuchochea vita zaidi na kuliteketeza eneo zima la Mashariki ya kati. Jordan, Pakistan, Umoja wa Falme za kirabu, Ujerumani na Uingereza ni miongoni mwa mataifa yaliyotaka juhudi za kidiplomasia kuchukuliwa kupoza kitisho cha usalama katika eneo hilo.
Shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya atomiki IAEA linapanga kukutana wiki ijayo na bodi ya magavana wake mjini Vienna kufuatia ombi la Iran kutokana na shambulizi lililofanyika hii leo. Bodi hiyo awali iliikosoa Iran kutoshirikiana na wakaguzi wake katika ukaguzi wa vinu vyake vya nyuklia.
reuters, ap, afp