Israel inatanua operesheni Gaza ili kuteka 'maeneo makubwa'
2 Aprili 2025Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz amesema mashambulizi ya Israel huko Gazayanatanuliwa ili kuangamiza na kuwafurusha wanamgambo katika eneo hilo. Aidha amesema watakamata maeneo makubwa ambayo yataongezwa kwenye sehemu za kiulinzi za Taifa la Israel.
Serikali ya Israeli kwa muda mrefu imedumisha eneo la ulinzi ndani ya Gaza kando ya uzio wake wa usalama na eneo hilo limetanuka sana tangu vita ilipoanza mwaka 2023.
Israel inasema eneo hilo la ulinzi linahitajika kwa ajili ya usalama wake, wakati Wapalestina wanaliona kuwa unyakuzi wa ardhi ambao unaupunguza kwa kiasi kikubwa ukanda huo mwembamba wa pwani, ambao ni nyumbani kwa watu milioni mbili.
Katz hakufafanua maeneo ya Gaza ambayo yatanyakuliwa kwenye operesheni hiyo iliyotanuliwa, ambayo alisema yanajumuisha zoezi la kuhamisha idadi kubwa ya watu wanaoishi kwenye maeneo ya mapigano. Matamshi yake yamejiri baada ya Israel kuamuru wakaazi kuhama mji wa kusini wa Rafah na maeneo yaliyokaribu.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amerudia miito kwa Hamas kusalimisha silaha akisema matumizi ya shinikizo la kijeshi ndio njia pekee ya kuwarejesha nyumbani mateka 59 waliobaki. "Kuanzia sasa, Israel itachukua hatua dhidi ya Hamas kwa nguvu kubwa, na kuanzia sasa na kuendelea, mazungumzo yatafanyika tu wakati mashambulizi yakiendelea. Hamas tayari wamehisi uzito wa nguvu yetu katika saa 24 zilizopita, na ninataka kuwahakikishia huu ni mwanzo tu."
Israel iliendelea kuilenga Gaza, huku mashambulizi ya angani ya usiku kucha yakiwauwa watu 17 katika mji wa kusini wa Khan Younis.
Watu wengine 15 waliuawa kwenye shambulizikaskazini mwa ukanda huo kwa mujibu wa maafisa wa hospitali ambazo miili hiyo ilipelekwa. Watu hao wakiwemo watoto tisa waliuawa kufuatia shambulizi kwenye jengo la ofisi za SHirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina – UNRWA katika kambi ya wakimbizi ya Jabaliya. Niur Bakir, ni mmoja wa wakazi waliopoteza makaazi. "Hali hii itaendelea hadi lini? tumechoka. Wanasema sisi ni wastahimilivu? Hatuna ustahimilivu, tunakufa, tunaangamia kwenye dunia hii. Waache watuangamize na kutupunguzia mateso, tumechoka. Je, haya yataendelea hadi lini?"
Nayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imesema Wajerumani 19 wamefanikiwa kuondoka Gaza Pamoja na jamaa zao wa karibu baada ya mazungumzo na maafisa wa Israel. Taarifa ya wizara hiyo imesema raia hao waliondoka Gaza kwa kutumia kivuko cha mpakani cha Kerem Shalom. Kisha walitumia ndege kutoka kusini mwa Israel na kuelekea Ujerumani moja kwa moja.