Israel inafanya jinai ya kimbari Gaza - wasomi
1 Septemba 2025Miripuko mikubwa na milio ya risasi ilisikika kwenye eneo zima la Jiji la Gaza usiku wa kuamkia Jumatatu (Septemba 1), wakati jeshi la Israel likiendeleza mashambulizi yake kwenye jiji hilo ambalo wiki iliyopita ililitangaza rasmi kuwa "uwanja wa kivita."
Jeshi hilo liliwataka malaki ya Wapalestina wanaoshi kwenye jiji hilo kukimbilia upande wa kusini, lakini wengi ama wanasema wameshaishiwa na nguvu baada ya kuhamishwa mara kadhaa au wanaonesha kutokushawishika kwamba kuna mahala popote palipobakia salama ndani ya Ukanda huo mzima.
Zaidi ya asilimia 90 ya wakaazi zaidi ya milioni mbili wa Gaza wameshawahi kuhamishwa angalau mara moja ndani ya kipindi cha miezi 23 ya vita, huku wengi wao wakiwa wameshahamishwa mara nyingi zaidi, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Israel imeashiria kwamba kiwango cha misaada inayoingia kwenye Ukanda huo kinaweza kupunguzwa, na imetangaza ujenzi wa miundombinu mipya kusini mwa Gaza - hatua ambazo Wapalestina wanasema zinalingana na kuwafukuza watu kwa mabavu.
"Kinachotendeka Gaza ni jinai ya kimbari"
Siku ya Jumatatu, jumuiya ya wasomi wakubwa juu ya masuala ya mauaji ya kimbari ulimwenguni ilipitisha azimio lililosema kwamba vigezo vya kisheria vinathibitisha kuwa Israel inaendesha jinai ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Asilimia 86 ya waliopiga kura miongoni mwa wajumbe 500 wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wasomi wa Kimbari waliunga mkono azimio hilo, ambalo linatangaza kwamba: "Sera na matendo ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza yanakidhi fasili ya kisheria ya mauaji ya kimbari kwenye Kifungu cha Pili cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Uzuiaji na Adhabu ya Jinai ya Kimbari wa mwaka 1948."
Hakukuwa na jibu la haraka kutoka wizara ya mambo ya kigeni ya Israel baada ya kutolewa tamko hilo mjini The Hague, Uholanzi, lakini daima Tel Aviv imekuwa ikipinga vikali kwamba matendo yake huko Gaza ni jinai ya kimbari na imekuwa ikipambana kwenye Mahakama ya Haki ya Kimataifa dhidi ya kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini.
Wahouthi washambulia 'meli ya mafuta ya Israel'
Hayo yakijiri, jeshi la Wahouthi nchini Yemen lilisema siku ya Jumatatu kwamba lilikuwa limeishambulia meli ya mafuta ya Israel kwenye Bahari ya Shamu, ikiwa ni sehemu ya kampeni yake ya kuonesha mshikamano na Wapalestina.
Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo kupitia chaneli ya Telegram ilisema meli ya Scarlet Ray ilishambuliwa ikiwa kaskazini mwa Bahari ya Shamu.
Mtandao unaofutillia safari za meli, Vesselfinder, ulisema meli hiyo ilikuwa inapeperusha bendera ya Liberia.
Siku ya Jumapili (Agoti 31), Shirika la Operesheni za Biashara Baharini la Uingereza (UKMTO) liliripoti kupokea taarifa kutoka kwa manahodha wa meli moja wakisema kulikuwa kumetokea mripuko karibu na meli yao iliyokuwa kusini magharibi mwa Yanbu, Saudi Arabia.