Israel inaendeleza mashambulizi yake Ukanda wa Gaza
14 Julai 2025Kwa mujibu wa msemaji wa ulinzi wa raia Mahmoud Bassal aliyezungumza na shirika la habari la AFP, waPalestina kumi waliuawa kwenye mashambulizi matatu tofauti ya angani yaliyoyalenga maeneo mbalimbali ya mji wa Gaza upande wa kaskazini. Watu wengine 12 waliuawa eneo la kusini la Khan Younis. Kwa upande wake, jeshi la Israel limesema linafuatilia taarifa hizo.
Kulingana na taarifa ya jeshi,vikosi vya Israel viliharibu majengo na miundo mbinu ya kigaidi inayotumiwa na wapiganaji wa Hamas na wale wa Palestinian Islamic Jihad kwenye maeneo ya Gaza ya Shujaiya na Zeitun. Walioachwa bila makazi walilazimika kuhama tena baada ya jeshi la Israel kurejea kwenye eneo la kusini mwa Gaza la Khan Younis,limeripoti shirika la habari la Palestina la Wafa. Belal Al Adlouni alimpoteza kaka yake kwenye mashambulio ya anga na anasikitika sana.
"Hakuna makubaliano yoyote ya kusitisha vita kati yetu na wao, kila tone la damu litalipiziwa kisasi na kamwe halitasahaulika na kumalizwa na muda,au kuhangaishwa au kifo.Tuko hapa sasa na kisasi chetu kitalipiziwa si tu mashujaa wetu bali pia kwa kila tone la damu la mtoto, shujaa na aliyedhulumiwa," alisema Belal.
Kwa upande wake, ripoti ya tarehe 9 Julai ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, zaidi ya asilimia 86 ya eneo la Ukanda wa Gaza liko chini ya usimamizi wa jeshi la Israel na makaazi ya muda.Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaashiria kuwa zaidi ya watu laki 725 wameachwa tena bila makaazi tangu makubaliano ya kusitisha vita kukiukwa katikati ya mwezi wa Machi.
Mazungumzo ya amani Gaza yatatizwa na misimamo ya Israel
Yote hayo yakiendelea,mazungumzo ya kusaka amani yanayosuasua yameingia wiki yake ya pili. Duru za kuaminika zinaeleza kuwa Hamas imepinga mapendekezo ya kuweka vikosi kwenye eneo la ukubwa wa asilimia 40 ya Gaza pamoja na mipango ya kuwahamisha waPalestina kwenye kizio maalum mpakani na Misri.Kwa upande wake, shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina, UNRWA, imeuelezea mpango huo kuwa kambi ya mateso nayo Idara ya usalama ya Israel inaripotiwa kutofurahishwa na mipango hiyo.