Hamas: Israel inajaribu kuwaua kwa njaa watu wa Gaza
17 Aprili 2025Kundi la Hamas kwenye taarifa yake limesema hatua ya Israel ya kuanza tena kuzuia misaada kuingiaUkanda wa Gaza inadhihirisha waziwazi ya kwamba taifa hilo linafanya uhalifu wa kivita, ambao ni pamoja na kutumia njaa kama silaha na kuzuia bidhaa muhimu kama dawa, maji na mafuta kuwafikia watu wasio na hatia kwa wiki ya saba mfululizo.
Israel ilitangaza kuendeleza hatua hiyo iliyodumu kwa wiki sita sasa. Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz alisema jana Jumatano kwamba zuio hilo ni mojawapo ya "mbinu za shinikizo zaidi dhidi ya Hamas, ambao Israel inawashutumu kwa kuichukua misaada hiyo badala ya kuwafikia walengwa, ili kuendeleza udhibiti wake.
Soma pia:Netanyahu asema kuundwa dola la Wapalestina ni sawa na ''kuuzawadia ugaidi''
Kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayojishughulisha na misaada ya kiutu, OCHA, karibu watu wote wa Gaza kwa sasa wanategemea chakula kinachoandaliwa kwenye majiko ya umma, yanayosaidiwa na mashirika ya misaada.
Namna nyingine ya kupata chakula kwenye eneo hilo, ni kutoka kwenye masoko. Lakini, ni bahati mbaya kwamba wengi wao hawawezi kununua kwa sababu ya ongezeko kubwa la bei, huku bado kukishuhudiwa upungufu mkubwa.
Hii inamaanisha kwamba misaada ya kiutu ndio njia pekee kubwa ya kuwezesha upatikanaji wa vyakula kwa ajili ya asilimia 80 ya watu wa Gaza, hii ikiwa ni kulingana na Mpango wa Chakula Ulimwenguni, WFP kwenye ripoti yake ya mwezi Aprili kuhusu masoko ya Gaza.
Soma pia: Umoja wa Ulaya kutoa Euro bilioni 1.6 kwa Palestina
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephanie Tremblay amesema jana Jumatano kwamba pamoja na kitisho cha njaa, karibu nusu milioni ya watu wa Gaza wameyakimbia makazi yao tangu Machi 18, wakati Israel ilipoanzisha upya mashambulizi dhidi ya Hamas. Amesema umoja huo kwa sasa unashindwa kabisa kusambaza mahema kwa ajili ya watu hao kutokana na vizuizi vilivyowekwa na Israel.
"Uhasama katika Ukanda wa Gaza unaendelea kuathiri vibaya raia, na kusababisha vifo zaidi, watu kukimbia na uharibifu wa miundombinu muhimu. Washirika wetu wa kibinadamu wanakadiria kuwa tangu Machi 18, karibu watu nusu milioni wamelazimika kuhama au kufukuzwa kwa mara nyingine tena. Wanatuambia, haiwezekani tena kusambaza mahema kwenye eneo la Gaza."
Tukigeukia uwanja wa mapambano, taarifa kutoka idara ya usalama wa umma za Gaza zimesema mapema leo kwamba Israel imefanya mashambulizi ya angani na kushambulia kambi nyingi za Wapalestina waliokimbia makazi yao katika eneo hilo, pamoja na kuua watu wasiopungua 25.
Msemaji wa idara hiyo Mahmud Bassal amesema mashambulizi hayo ya usiku wa jana yalilenga baadhi ya mahema katika eneo la Al-Mawasi, kusini mwa mji wa Khan Yunis na kuua watu 16, wengi wao wakiwa ni kina mama na watoto, huku watu wengine 23 wakiwa wamejeruhiwa.
Bassal amesema, mashambulizi mengine mawili kwenye kambi za watu waliokimbia makazi yao yalisababisha vifo vya watu wanane na kuwajeruhi wengine kadhaa.
Soma pia:Hamas yatathmini pendekezo jipya la kusitisha mapigano Gaza